SERIKALI YATOA TAARIFA KUHUSU TISHIO LA KUVAMIWA NA NZIGE


  UTANGULIZI
Ndugu Wanahabari,
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoweza kuathirika na aina mbili za Nzige yaani Nzige Wekundu na Nzige wa Jangwani. Kutokana na athari za milipuko ya Nzige iliyotokea miaka ya 1929 hadi 1944 kwa Nzige wekundu na miaka ya 1960 kwa Nzige wa Jangwani, Tanzania ilichukua uamuzi wa kujiunga na Mashirika mawili ya Udhibiti wa Nzige. Mashirika hayo ambayo yanatambuliwa na Umoja wa Mataifa ni Shirika la Kudhibiti Nzige wa Jangwani la Mashariki mwa Afrika (Desert Locust Control Organization for Eastern Africa – DLCO EA) na Shirika la Kudhibiti Nzige Wekundu la Kusini na Kati mwa Afrika (International Red Locust Control Organization for Central and Southern Africa – IRLCO-CSA).



Ndugu Wanahabari,
Mwanzoni mwa mwezi Januari, 2020 Shirika la Kimataifa la Nzige wa Jangwani la Mashariki mwa Afrika lilitoa taarifa ya kuwepo kwa makundi ya Nzige wa Jangwani kwenye Nchi jirani ya Kenya maeneo ya Sambulu, Isiolo, Kakamega, Embu, Meru, Tana River na Turkana. Aidha, wiki hii imeripotiwa kuwa makundi ya Nzige wa Jangwani yameonekana eneo la Karamoja umbali wa Kilomita 166 kutoka mpaka wa Uganda. Nzige wa Jangwani wanaathari kubwa katika uzalishaji wa mazao ya chakula na malisho ya mifugo. Kundi moja la Nzige lina uwezo wa kuruka bila kutua kwa umbali wa Kilomita 150 kwa siku.

 Nzige mmoja ana wastani wa uzito wa gramu mbili (2) na wana uwezo wa kula sawa na uzito wake kwa siku. Kundi la Nzige lina wastani wa Nzige wapatao Milioni 40 kwenye eneo la Kilomita Moja za Mraba na hivyo huweza kusababisha upotevu wa uoto  takribani tani 80 kwa siku katika eneo hilo. Katika hatua ya tunutu (panzi wadogo), Nzige hudhibitiwa kwa kunyunyuzia kiuatilifu maalum kwa usimamizi wa wataalam; na katika hatua ya ukomavu ambayo mara nyingi nzige huwa katika makundi makubwa yanayodhibitiwa kwa kunyunyuzia kiuatilifu kwa kutumia ndege.

    HALI ILIVYO SASA
Ndugu Wanahabari

Tangu kuripotiwa kwa uwepo wa Nzige wa Jangwani katika Nchi za Eritrea, Ethiopia, Somalia, Sudan na Kenya, Serikali ya Tanzania pia imeendelea kupata taarifa za viashiria vya kuwepo kwa visumbufu vya Nzige wa Jangwani kupitia mitandao ya kijamii, simu na taarifa za utabiri za Mashirika ya Kimataifa. Kufuatia taarifa hizo, Wizara kwa kushirikiana na Wataalam wa Shirika la Nzige wa Jangwani, Wataalam ngazi za Mikoa na Halmashauri imeendelea kufuatilia taarifa hizo.

Hadi sasa, hakuna uthibitisho wa kitaalam kuhusu uwepo wa Nzige wa Jangwani hapa nchini.

    HATUA ZINAZOENDELEA KUCHUKULIWA NA SERIKALI
Ndugu Wanahabari,

Kwa kutambua athari za visumbufu vya milipuko, Serikali kila mwaka hutenga fedha za kukabiliana na milipuko ya visumbufu vya mazao na mimea vinavyoweza kujitokeza. Visumbufu hivyo ni pamoja Nzige wa Jangwani, Nzige Wekundu, Ndege waharibifu wa Nafaka aina ya Kwelea Kwelea, Panya na Kiwavijeshi Vamizi. Kutokana na taarifa za kuwepo kwa tishio la kuvamiwa na Nzige wa Jangwani hapa nchini, Serikali inaendelea kuchukua tahadhari kwa kufanya yafuatayo:-
  1.     Kuratibu upatikanaji wa viuatilifu maalum vya kudhibiti Nzige,kwa sasa kuna jumla ya lita 7,000 kwa ajili tahadhari. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inaendelea na manunuzi ya viuatilifu kwa ajili ya kudhibiti nzige na visumbufu vingine vya mlipuko.
  2.     Wizara imewatuma wataalam katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Mara ambayo inapakana na nchi jirani ya Kenya kufuatilia na kubaini viashiria vya uwepo wa Nzige wa Jangwani.
  3.     Kuandaa Mpango wa kukabiliana na tishio la kuvamiwa na Nzige wa Jangwani utakaozishirikisha Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali, Mashirika ya Kimataifa, Sekta Binafsi na wakulima.
  4.     Kuendelea kutoa elimu ya utambuzi na Udhibiti wa Nzige wa Jangwani kwa wadau wa kilimo wakiwemo wakulima na Maafisa Ugani katika maeneo mbalimbali nchini kupitia mafunzo maalum, vipindi vya Radio, TV na mitandao ya kijamii.
  5.     Kuandaa machapisho kwa lugha rashisi mfano vijarida, vipeperushi na miongozo ya kudhibiti Nzige wa Jangwani.
    WITO KWA WANANCHI NA WADAU WA KILIMO
Ndugu Wanahabari,

Kama nilivyotangulia kusema, Nzige wa Jangwani wana athari kubwa katika uzalishaji wa mazao ya kilimo, malisho ya mifugo na uoto wa asili. Uwepo wa Nzige hao katika Nchi Jirani unatulazimu kama nchi kuchukua tahadhari mapema ili kukabiliana na tishio hilo.

Pamoja na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali, napenda kutoa wito kwa wananchi hususan wakulima na wadau wengine wa kilimo kushirikiana na Serikali kwa kufanya yafuatayo:-
  1.  Kutoa taarifa ya viashiria au uwepo wa Nzige wa Jangwani kwenye maeneo ya kilimo, malisho na uoto wa asili kupitia Uongozi wa Kijiji, Kata, Wilaya, Mkoa na Wizara ya Kilimo.
  2.   Wakulima kutoa ushirikiano kwa wataalam wa Wizara ya Kilimo, Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Halmashauri katika hatua mbalimbali za tahadhari na udhibiti wa Nzige endapo watatokea.
  3.   Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwasimamia Maafisa Ugani waliopo kwenye maeneo yao ili kuhakikisha kwamba wanawatembelea wakulima mashambani na kubaini endapo kuna viashiria vya uwepo wa Nzige.
  4.   Tunaomba Wabia wa Maendeleo, Taasisi mbalimbali za umma na sekta binafsi kushirikiana na Wizara ya Kilimo kutekeleza Mpango wa Kukabiliana na Tishio la Nzige ili kuhakikisha kwamba nchi yetu inaendelea kuwa na uhakika wa chakula na wakulima kupata kipato chao kutokana na shughuli zao za kilimo.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA.
Japhet N. Hasunga (Mb.)
WAZIRI WA KILIMO
29 JANUARI, 202


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post