Bi. Siri Yasini Swedi
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Kujiamini ndiyo silaha kubwa kwa mwanamke kufanikiwa katika masuala ya uongozi!!! Hii ni kauli ya Bi. Siri Yasini Swedi aliyetumikia uongozi katika Chama Cha Demokrasia na Maendeleo mkoani Shinyanga kwa kipindi cha miaka 17 na sasa ni Mwenyekiti wa Chama Cha ACT Wazalendo mkoa wa Shinyanga tangu mwaka 2015.
Siri Yasini Swedi ni mama mwenye watoto wanne,ameolewa alizaliwa mwaka 1974 katika kata ya Kambarage halmashauri ya wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga.
Siri Yasini alianza kujihusisha na masuala ya siasa mwaka 1998 akiwa binti wa miaka 24.
Akizungumza na Malunde 1 blog, Siri Yasini amesema mwaka 1998 akiwa mfanyabiashara wa mihogo na nafaka katika soko la Nguzo Nane Mjini Shinyanga wakati Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikiwa katika harakati za kutafuta wanachama,alishawishiwa kuwa mwanachama wa CHADEMA akakubali na ndiyo safari yake katika masuala ya siasa ilipoanzia.
Siri Yasini anasema baada ya kuwa mwanachama,mwaka huo huo 1998 alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA)wilaya ya Shinyanga hadi mwaka 2000.
“Ukishakuwa Mwenyekiti wa wilaya unakuwa Mjumbe wa Baraza Kuu CHADEMA na Mjumbe wa Mkutano Mkuu CHADEMA taifa”,anaeleza Siri Yasini.
“Nikiwa Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Shinyanga, Mwaka 1999 wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa nilichaguliwa kuwa Mjumbe wa serikali ya mtaa wa Tanesco kata ya Chamaguha katika Manispaa ya Shinyanga kupitia CHADEMA. Wakati huo kulikuwa na shida kidogo kwani chama kilikuwa bado kidogo na watu walikuwa hawakielewi elewi.
Nilitumikia nafasi ya ujumbe wa serikali ya mtaa hadi mwaka 2004”,anasimulia Siri Yasini.
“Mwaka 2000 kwenye uchaguzi Mkuu wa CHADEMA,nilifanikiwa tena kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Shinyanga.Tuligombea wanne ambapo wanaume walikuwa watatu,mwanamke nilikuwa peke yangu,nikashinda.Nimeitumikia nafasi hiyo hadi mwaka 2005”,anasema Siri Yasini.
Anabainisha kuwa hata kwenye uchaguzi mkuu wa CHADEMA mwaka 2005 aligombea tena nafasi hiyo akichuana na wanaume wawili kutokana na uimara wake katika masuala ya siasa akachaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Shinyanga kwa miaka mitano mingine hadi mwaka 2010.
Mnamo mwaka 2010 Siri Yasini aliingia kwenye Kinyang’anyiro cha Udiwani kwenye kura za kuchaguliwa ndani ya chama kata ya Chamaguha akapata nafasi ya pili akigombea na wanaume wawili na baada ya kushindwa akateuliwa kuwa Diwani wa Viti Maalumu kata ya Chamaguha mpaka mwaka 2015.
Hata hivyo baada ya Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Shinyanga Philip Shelembi mwaka 2011 Siri Yasini aliteuliwa kushikilia nafasi ya Mwenyekiti mkoa kwa muda hadi muda wa uchaguzi alipochaguliwa mwenyekiti mwingine.
Mwaka 2015 Siri Yasini alihama CHADEMA na kwenda Chama Cha ACT Wazalendo na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho cha ACT Wazalendo nafasi ambayo anaitumikia mpaka sasa.
NINI SIRI YA SIRI YASINI KUFANIKIWA KUWA KIONGOZI WA KISIASA MWANAMKE KWA MUDA WA MIAKA 25 MFULULIZO?
Siri Yasini anasema licha ya kubezwa kuwa mwanamke hawezi kuwa kiongozi,kitu cha msingi alichokisimamia yeye kama mwanamke na hatimaye kufanikiwa katika uongozi wa kisiasa ni kujiamini na kutofanya kazi kinadharia.
“Siasa inaongozwa na katiba.Kwa hiyo ni vizuri sana ukaielewa Katiba na Ilani ya Uchaguzi ya Chama chako cha siasa. Unapoenda kwenye majukwaa yako ni vyema pia ukapitia katiba ya Nchi, na kupitia vitu vinayoleta shida ndani ya nchi ama kwenye eneo unalotaka kugombea uongozi. Lazima ujue vitu vya kila siku ambavyo unaishi navyo ndipo utajiamini.
“Unapoenda kusema kitu usiseme kwa kufikiri,jaribu kukifanyia utafiti kwanza uone kama kina ukweli ndani yake au la! Halafu ndiyo nenda ukaseme. Ukweli ndiyo utakufanya ujiamini. Usipojiamini anaweza kutokea mtu akakuuliza kitu kidogo tu ukababaika.
Usikae sehemu moja ukajifungia maana yake hautajua changamoto kwani chama cha siasa hususani cha upinzani kinaangalia changamoto ambazo zipo ndani ya serikali inayoongoza.Ni vizuri ukafuatilia hizo changamoto ukaujua ukweli. Fanya utafiti, ujiridhishe vinginevyo wananchi watakushangaa kuzungumzia vitu ambavyo havipo kwenye eneo lako”,anafafanua Siri Yasini.
Kuhusu Matumizi ya pesa nyingi ili kufanikiwa katika siasa, Siri Yasini anasema:
“Kwa kweli katika nafasi za uongozi nilizopitia sijatoa pesa kabisa. Nilikuwa nasimama na kunadi sera zangu na nikapewa kura licha ya maneno mengi mtaani ‘Mwanamke hana hela atakuwa malaya,wakubwa hawatamuacha’. Siasa ina maneno mengi sana ya kukatisha tamaa,Huwezi kumzuia mtu kusema. Mimi nilikuwa naujua ukweli wangu ni nini,nilisimamia ukweli wangu ndiyo maana nilifanikiwa kusimama mpaka hapa nilipo leo”,amesema Siri Yasini.
CHANGAMOTO GANI KAPITIA?
Siri Yasini anasema changamoto kubwa aliyopitia ni kubezwa ambapo jamii ilimbeza sana ambapo wengine walibeza umri wake mdogo (umri miaka 24) kupewa dhamana ya kuongoza chama.
“Changamoto zingine zinakuwa ndani ya chama,wapinzani unaogombea nao nafasi za uongozi.Kuna wengine wanaamua kukuchafua tu na kipindi hicho nilianza uongozi nikiwa binti mdogo umri wa miaka 24.Kipindi hicho vijana wachache walikuwa wanapata nafasi za uongozi.
Wengine walikuwa wanasema ‘mmempa huyu binti uongozi atakiharibu chama’ lakini mwisho wa siku wakiangalia utendaji kazi wako inabidi tu wakubaliane na wewe. Kuna maneno mabaya kabisa ambayo kwa kweli hayaleti picha nzuri”,amesema Siri Yasini.
RAI YA SIRI YASINI KWA WANAWAKE
Siri Yasini anawasisitiza wanawake wanaotaka kugombea nafasi za uongozi kuacha kuoga,wajiamini na kupuuza wanaowabeza kwani Uongozi ni Busara, Akili wala siyo Misuli akibainisha kuwa wanaume sasa wanawafurahia wanawake wachapakazi na wanaojiamini ndiyo maana yeye amekuwa kiongozi Mwanamke ndani ya CHADEMA na ACT Wazalendo na wanaume na wanawake wanapenda utendaji kazi wake ndiyo maana hadi sasa ni kiongozi.
“Kutokujiamini kuna mambo mengi ikiwemo kuwaza kuwa mimi nikienda nani ataniunga mkono ‘nani atani sapoti’ sina hela mkononi,nitasimamaje jukwaani na mambo mengine mengi ambayo yanamsababisha hata hamu ya kugombea inafifia.Hutakiwi kuwaza hayo unachotakiwa kuwaza ni kuona unaweza kufanya nini kwa sababu unajiamini”,amesema.
Hata hivyo anasema mila na desturi za kwamba mwanamke hawezi kuongoza zimepitwa na wakati kwani sasa jamii ina uelewa na wanawake viongozi wanapewa heshima kama wanavyopewa wanaume na wanawake viongozi wamekuwa na mashabiki wa kike na wa kiume.
“Uoga ni tatizo kubwa sana kwa wanawake kutothubutu kugombea nafasi za uongozi. Uoga mwingine unatokana na kubezwa kuanzia ndani ya familia,wanawake wengi wanakatishwa tamaa ndani ya familia zao.
Hata mme wako anaweza kukubeza lakini ukisimama vizuri huyo atakuwa shabiki wako namba moja na atakusaidia kushawishi na kukutafutia kura kwa wanaume wenzake na jamii kwa ujumla. Hakuna mtu anamuunga mkono mtu muoga, hivyo wanaotaka uongozi wasiwe waoga wajiamini”,anasema Siri Yasini.
NINI USHAURI WA SIRI YASINI KWA JAMII?
Siri Yasini anaiomba jamii kuwapa ushirikiano ‘sapoti’ wanawake kwa sababu kwanza wanawake wanaweza kufanya mambo makubwa.
“Kupitia mimi nimeona wanawake wanafanya mambo makubwa.Nikiwa Mwenyekiti wa CHADEMA hapa wilaya ya Shinyanga Mjini nilikuta wenyeviti wa vitongozi wawili mmoja alikuwa Negezi Mwawaza na mwingine Mpera A Ibadakuli,lakini baada ya kuwa kiongozi ndani ya miaka mitano nikapata viongozi wanawake zaidi ya 20 na katika uongozi wangu hatujawahi kushuka,wanawake wameendelea kujitokeza kugombea nafasi za uongozi hadi ngazi ya Udiwani na Majimbo na mimi nikiwa mfano wao”,amesema Siri Yasini.
Siri Yasini anaishukuru jamii sasa kwa kuendelea kuwaamini na kuwapa nafasi za uongozi wanawake tofauti na siku za nyuma ambapo wanawake walikuwa hawapewi nafasi za uongozi akidai kuwa hata yeye wakati alipopewa nafasi kuongoza CHADEMA wilaya ya Shinyanga Mjini jamii ilikuwa inamshangaa na kuona kama jambo la ajabu mwanamke kuongoza jamii.
“Siku za nyuma ilikuwa changamoto,wanaume walikuwa wanashangaa sana kuniona mwanamke napanda jukwaani,walikuwa wanashtuka sana kusikia sauti ya mwanamke kwenye majukwaa ya siasa.Wengine walikuwa wanakuja kwenye mikutano kunishangaa tu nikiwa jukwaani. Mwanamke anasimamaje Jukwaani? Walikuwa wanawaza kuwa mwanamke hawezi. Walivyonisikiliza na kunielewa wakanikubali na wakawa mashabiki zangu”,anasimulia Siri Yasini.
WITO WA SIRI YASINI KWA WANAWAKE WANAOTAKA UONGOZI.
Siri Yasini anawaomba wanawake wajitokeze kwa wingi kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea nafasi za uongozi (Udiwani,Ubunge na Urais) katika Uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka huu 2020.
“Mwanamke anaweza kuwa diwani mzuri kabisa,anaweza kuwa Mbunge mzuri na akaongoza Jimbo lake vizuri kabisa.Tunaona kuna wabunge wengine majimbo yao yamewashinda lakini nafasi hiyo akipewa mwanamke mabadiliko makubwa lazima yaonekane”,amesema Siri Yasini.
“Nawasihi wanawake wajitokeze kuchukua fomu kugombea nafasi za uongozi katika Jimbo la Shinyanga Mjini. Natamani angetokea mwanamke mwenye uwezo,anayejitambua,mwenye kuweza kutetea na kujenga hoja vizuri.
Naomba wananchi wa Shinyanga wafanye hivyo kwani haijawahi kutokea Mwanamke kuwa kiongozi wa jimbo ni vizuri safari hii tukaamua kubadilisha tuweke mwanamke ili tuweze kutoka hatua moja kwenda nyingine.Wachukue fomu na watafanikiwa.
Mwanamke akishika nafasi huwa panaonekana kweli pameshikwa .Mwanamke ni mtu anayejituma,mwanamke ni mtu mwenye misimamo,ni mtu mwenye nidhamu siyo nidhamu ya uoga,ana nidhamu ya kitu anachokifanyia kazi”,anaeleza Siri Yasini.
Amesema Chama Cha ACT Wazalendo kimejipanga vizuri katika chaguzi zake za ndani na Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 na kwamba agizo kubwa la Chama ni kuhakikisha wanawake wengi wanachukua fomu za kugombea za uongozi na tunaendelea kufanya mikakati ya kuwafikia wapiga kura na kuwaeleza kuwa mwanamke anao uwezo wa kuongoza vizuri.
“Katika chama chetu cha ACT Wazalendo tunaendelea na mkakati mkubwa wa kuhamasisha wanawake kugombea nafasi za uongozi na nyinyi vyombo vya habari ni sehemu ya sauti yetu kutushika mkono ili tufikie malengo yetu tunayoyafikiria”,amesema.
NDOTO YAKE NI NINI 2020?
Siri Yasini ambaye amekuwa kiongozi wa vyama vya siasa kwa takribani miaka 25 sasa, anasema ndoto yake kubwa mwaka 2020 ni kugombea Ubunge katika Jimbo la Shinyanga Mjini na anawaomba Watanzania kumuunga mkono pindi muda utakapowadia kwani uwezo wa kuongoza anao na anajiamini.
Katika Uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2019 inaelezwa kuwa wanawake katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga hawakujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi na kusababisha kupata viti vichache kwenye uongozi.
Msimamizi wa uchaguzi wa Serikali za mitaa manispaa ya Shinyanga Charles Kafutila anasema matokeo ya uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2019 katika manispaa ya Shinyanga kuna vijiji 17, lakini hakuna mwanamke aliyeshinda hata kiti kimoja, kwenye mitaa 55 wanaume walishinda viti 49 wanawake viti sita, vitongoji 84, wanaume walishinda viti 76 na wanawake viti nane.
Septemba 27,2019, TGNP Mtandao kwa kushirikiana na Taasisi ya Women Fund Tanzania na Mtandao wa Wanawake na Katiba,Uchaguzi na Uongozi ulizindua Ilani ya Uchaguzi ya Wanawake ya Uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka 2020.
Ilani ya uchaguzi ya wanawake ya mwaka 2019/2020 imeweka masuala muhimu ya jinsia katika uchaguzi na inazitaka mamlaka zote kuzingatia masuala ya jinsia katika uchaguzi.
Ilani hiyo pia inataka wadau wote wa uchaguzi kuzingatia misingi ya ushindani wa haki na huru na usawa wa jinsia kama ilivyoainishwa kwenye katiba,sheria,sera,mipango ya nchi na kubainishwa kwenye mikataba ya kimataifa na kikanda ambayo serikali yetu imeridhia.
Social Plugin