Sultani Qaboos bin Said wa Oman aliyeitawala nchi hiyo kwa karibu nusu karne amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 79.
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Oman, ONA, siku tatu za maombolezo ya kitaifa zimetangazwa kufuatia kuaga dunia mfalme huyo .
Aidha bendera ya Oman itapepea nusu mlingoti kwa muda wa siku 40 kama heshima kwa kiongozi huyo ambaye anapongezwa na wengi kwa kuleta maendeleo na ufanisi mkubwa katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Kiongozi huyo wa Oman aliyeaga dunia alikuwa anaugua saratani ya utumbo mpana ambayo kwa lugha ya Kiingereza inaitwa 'colon cancer' au 'colorectal cancer'.
Mwezi Disemba Sultan Qaboos alielekea Ubelgiji kwa ajili ya matibabu na kisha akarejea nyumbani kabla ya kumalizika mwaka 2019.
Sultan Qaboos hakuwa na mtoto na wala hakutangaza bayana mrithi wa kiti chake lakini taarifa zinasema alikuwa ameandaa wasia kuhusu mrithi wake na akaukabidhi kwa Baraza la Ufalme.
Kwa mujibu wa katiba ya Oman, baada ya kifo cha Sultani, Baraza la Ufahame linapaswa kutangaza mrithi wake baada ya siku tatu. Baraza Kuu la Kijeshi la Oman tayari limeshaitisha kikao na kuitaka familia ya Sultan Qaboos itangaze mrithi wa kiti chake.
Sultan Qaboos alichukua hatamu za uongozi Julai 23 mwaka 1970 na anapongezwa kwa kufuata sera za kigeni zenye mlingano na hivyo kuiepusha Oman na migogoro.
Social Plugin