Meneja wa TMDA Kanda ya Kaskazini, Proches Patrick akizungumza kwenye mkutano huo.
*****
Na Andrew Chale - Arusha
MAMLAKA ya Dawa na vifaa tiba (TMDA) imekagua jumla ya shehena ya mizigo 3,160 ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya Forodha vilivyopo Kanda ya Kaskazini.
Meneja wa TMDA Kanda ya Kaskazini, Proches Patrick akizungumza ikiwa ni utekelezaji wa kampeni ya Tumeboresha sekta ya afya yenye lengo la kuonyesha mafanikio na mipango ya taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto.
Patrick alieleza kuwa, TMDA inatekeleza majukumu yake kisheria ambapo ukaguzi huo umefanyika katika mipaka ya Namanga, Holili, Tarakea pamoja na ule wa uwanja wa ndege wa KIA.
"Kwenye vituo vyote TMDA inawakaguzi na mfumo (IMIS) ambapo taarifa za vibali vya mizigo iliyokaguliwa huingizwa.".
"Katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya tano tumeweza kukagua shehena za mizigo 3,160 ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwenye vituo vya Forodha na mizigo ambayo haikukidhi vigezo vya ubora, usalama na ufanisi iliteketezwa na mingine kurudishwa kwenye nchi ilikotoka.
Lakini pia katika kipindi hicho, wametoa vibali mbalimbali na kuwa na ongezeko kubwa.
"Katika kipindi hiki ongezeko la maombi ya vibali vya kuingiza bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Jumla ya vibali 1,160 vilitolewa huu ni ushahidi tosha kuwa elimu ya udhibiti kwa wadau wetu imeeleweka na kukidhi sheria bila shuruti." Alisema.
Patrick ameongeza kuwa, uboreshaji wa mifumo imesaidia kwa kutoa vibali kwa wateja wake ndani ya siku moja baadala ya siku tatu ya awali
"Ikitokea sampuli haikukidhi vigezo hatua za haraka huchukuliwa kuondoa bidhaa husika sokoni, kwa matokeo ambayo hayakukidhi vigezo"alisema.
pia amesema wameweza kufanya ukaguzi wa bidhaa katika maeneo kama famasi, maduka ya dawa muhimu, maghala, hospitali, vituo vya afya na zahanati 5,017 yalikaguliwa katika halamashauri 21 zinazosimiwa na TMDA.
"Tumekagua na kusajili maeneo ya biashara 514, pia kufuatilia ubora na usalama wa bidhaa sokoni, vilevile katika miaka minne ya Dk. Magufuli tumechukua sampuli 427 na kufanyia vipimo" alisema.
Kwa upande wake, Mkaguzi wa Dawa TMDA Kanda ya Kaskazini, Titus Malulu alisema uelewa wa wananchi umekuwa mkubwa.
Ambapo wamekuwa wakitoa taarifa kwa bidhaa zilizowaletea madhara.
Katika upimaji wa dawa alisema wamekuwa wakifanya mara kwa mara hasa kwa kununua ambazo tayari zipo sokoni lengo kuendelea kufuatilia ubora wake.
"Kama tutabaini inashida tutapeleka katika maabara yetu ya ubora Dar es salaam na wakipata kuwa zinashida tunaziondoa haraka sokoni"alisema