Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERA YA USHIRIKA MSINGI WA MABADILIKO CHANYA YA SEKTA YA USHIRIKA



 Mkurugenzi mstaafu wa Rabo Foundation Netherlands Bw. Pierre Van Hedel akielezea namna Vyama vya Ushirika vinavyofanya kazi katika nchi ya Netherlands kwa lengo la kujifunza na kuongeza ujuzi katika maboresho ya Sera ya Ushirika ya Tanzania

 Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika wa Kifedha Bw. Josephat Kisamalala akieleza jambo wakati wa Warsha ya maboresho ya Sera ya Maendeleo ya Ushirika

 Mkurugenzi wa Mipango Ufuatiliaji na Tathmini wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Bw. Buji Bampebuye akifafanua jambo katika kikao cha Warsha ya kujadili maboresho ya Sera ya Ushirika (2002) kilichokuwa kikifanyika Mkoani Morogoro hivi karibuni
Mjumbe wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika wa
Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT) Bi. Anna Lupiano akieleza matarajio ya Vyama
katika maboresho ya Sera ya Maendeleo ya Ushirika

 Mshauri wa Kibiashara wa Shirika la Kimataifa lisilo la Kiserikali AGRITERRA Bw. Raymond Lyimo akitoa mada kwa wajumbe wa Warsha ya maboresho ya Sera ya Maendeleo ya Ushirika
 Mshauri wa Kibiashara wa Shirika la Kimataifa lisilo la Kiserikali AGRITERRA Bw. Mikidadi Waziri akitoa mada wakati wa Warsha ya maboresho ya Sera ya Ushirika

**

Mkurugenzi wa Mipango Ufuatiliaji na Tathmini wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) Bw. Buji Bampembuye amesema wadau wote wa Ushirika wakitekeleza majukumu yao ya Kiushirika kupitia dira na mwelekeo wa Sera ya Ushirika, ni dhahiri kwamba Sekta ya Ushirika itakuwa na mabadiliko chanya na yenye tija kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Warsha ya kujadili maboresho ya Sera ya Ushirika (2002) iliyoanza Jumanne 28 Januari, 2020 hadi 29 Januari 2020, Mkoani Morogoro.

“Ushirika ni moja ya nyenzo muhimu inayoweza kutumika nchini katika kuondoa umaskini na kuondokana na uchumi tegemezi. Hivyo, kwa kuimarisha Sera ya Ushirika tunajiwekea misingi imara ya kuendeleza Ushirika nchini,” alisema Bw. Bampebuye

Bw. Bambebuye amesema Tanzania tunaweza kujifunza mambo mengi mazuri kutoka kwenye nchi zilizofanikiwa katika Sekta ya Ushirika pia tunaweza kutumia tafiti zetu zilizowahi kufanyika na kuingiza yatakayoongeza chachu ya ukuaji wa Sekta ya Ushirika na kupata Sera itakayokuwa ikijibu Changamoto za wakulima na Wanaushirika kwa ujumla.

Mshauri wa Kibiashara wa Shirika la Kimataifa lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na masuala ya Ushirika nchini liitwalo AGRITERRA Bw. Mikidadi Waziri akitoa mada katika Warsha hiyo ameeleza kuwa Shirika hilo kama mdau wa Ushirika limekuwa likifanya kazi katika kuongeza msukumo wa Maendeleo katika Sekta ya Ushirika kupitia mafunzo kwa Vyama vya Ushirika ya Utawala Bora, Usimamizi wa Fedha na uhamasishaji.

Bw. Mikidadi alisema kuwa baadhi ya Changamoto zilizopo katika Sekta ya Ushirika ni pamoja na ushiriki mdogo wa vijana na wanawake hususan katika ngazi za uongozi za Vyama vya Ushirika. Hivyo, akashauri haya ni mambo ya msingi ya kuzingatiwa katika maboresho ya Sera ili kuhakikisha kuwa Sekta inakuwa endelevu na inatoa fursa za kiuchumi kwa makundi yote ya jamii zetu.

Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT) Bi. Anna Lupiano amesema uboreshaji wa Sera ya Ushirika unatoa matazamio ya kupata utendaji na utekelezaji wa majukumu utakaoenda kujibu changamoto mbalimbali za Sekta ya Ushirika.

Bi. Lupiano ametoa wito kwa Viongozi na Watendaji wa Vyama vya Ushirika kufuata na kutekeleza matakwa ya Sera mpya itakapokuwa tayari katika hatua za utekelezaji ili kuboresha na kuhakikisha uendelevu wa Vyama vya Ushirika.


--

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com