Mwenyekiti wa mtaa wa Shunu Japhet Kaliwa
Na Adela Madyane - Malunde 1 blog Kahama
Vijana 21 wenye umri chini ya miaka 18 wamejisalimisha kwa mwenyekiti wa mtaa wa Shunu uliopo kata ya Nyahanga halmashauri ya Mji wa Kahama Mkoani Shinyanga Japhet Kaliwa kutokana na matukio mbalimbali ya utekaji nyara wananchi kwa kutumia silaha za jadi na vitu vyenye ncha kali nyakati za usiku.
Akizungumza na Malunde 1 blog leo Alhamis Januari 16,2020, Mwenyekiti wa mtaa wa Shunu Japhet Kaliwa amesema tukio hilo limetokea baada ya kuendesha msako mkali mara tu alipoapishwa ili kuwatumikia wananchi wa mtaani kwake.
Mwenyekiti huyo wa mtaa amesema vijana hao waliamua kusalimu amri na kukabidhi vifaa walivyokuwa wakitumia kutekeleza matukio ya uhalifu kwa muda mrefu ambavyo ni mapanga, mikasi, bisibisi, plaizi na viwembe.
"Mwanzo wakati mimi ninaingia madarakani wananchi walikuwa wanaleta malalamiko kila siku kuhusu watu kunyang'anywa simu,kukatwa mapanga.Nilipoingia madarakani niliunda kamati ya ulinzi na usalama ya watu 16,tukaanza Operesheni ya kuwakamata hawa vijana wavunjivu wa amani",amesema Kaliwa.
“Kwa kwa kweli baada ya msako mkali unaoendelea katika mtaa wa Shunu dhidi ya wahalifu vijana 21 chini ya umri wa miaka 18 walijitokeza ofisini kwa lengo la kujisalimisha wakidai wamebadilika, hawatajihusisha na vitendo vya uhalifu tena. Kulingana na makubaliano yetu hayo waliofukuzwa shuleni kwa utovu wa nidhamu tumewarejesha wanaendelea na masomo yao,” amesema.
Amesema kati ya sababu zilizowafanya vijana hao kujikita katika vitendo vya uhalifu ni kutokana changamoto ya maisha duni majumbani mwao kutokana na hivyo kujiingiza katika makundi mabaya.
Kaliwa amesema miongoni mwa vijana hao watukutu ni pamoja na wanafunzi wa shule ya Msingi Shunu ambao walifukuzwa shule kutokana na hali hiyo na kuongeza kuwa kwa busara yake baada ya kuwakamata ofisi yake haikuona sababu ya kuendelea kuwashikilia badala yake imewaonya kwa kuwa walikiri kutotenda makosa tena na baadhi ya waliofukuzwa shule ofisi iliwaombea msamaha ili waendelee na masomo.
“Kutokana na hali hiyo kati ya vijana 21 watano tumewatafutia vibarua vya kulima mashamba ya watu na wengine kazi za kusomba matofali kwa kutumia Matera (Toroli) la kukokotwa na wanyama ili kutatua changamoto za kimaisha,” amesema Kaliwa.
Kaliwa amesema ataendesha mikutano ya mara kwa mara kwa wananchi wake kuanzia tarehe 18/01/2020 ili kutoa elimu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwaasa wazazi kukaa na watoto wao na kuwafundisha maadili mema huku akisema kuwa kipaumbele ni suala la ulinzi na usalama.
Social Plugin