Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AFARIKI DUNIA KWA KULA WALI NA PILIPILI

Wu Huayan alikuwa akila wali na pilipili ili aweze kuweka akiba ya kumwezesha kumtunza ndugu yake mgonjwa.

Mwanafunzi wa China ambaye amekula wali na pilipili kwa miaka mitano ili aweze kuweka akiba ya kumwezesha kumtunza ndugu yake mgonjwa amefariki, vyombo vya habari vya China vimeeleza.

Magumu yaliyokuwa yakimkabili Wu Huayan yaliishitua China baada ya picha za binti huyo, ambaye alikuwa na uzito wa karibu kilo 20, kuibuka mwaka jana.

Alilazwa hospitalini mwezi Oktoba mwaka 2019 alipokuwa na tatizo la kupumua.

Michango ilifurika kwa ajili ya kumsaidia kurudi katika afya njema, lakini kaka yake aliwaambia wanahabari kuwa alifariki siku ya Jumatatu.

Bi Wu aliliambia gazeti la Chongqing kuwa alivigeukia vyombo vya habari kwa ajili ya kuomba msaada baada ya kushuhudia baba na bibi yake wakifariki kwa kuwa hawakuwa na pesa za kulipa matibabu.

''Sitaki kushuhudia hayo tena -kusubiri kifo kwa sababu ya umasikini,'' alisema.

Kaka yake, ambaye hakutajwa jina lake, aliliambia gazeti la vijana la Beijing kuwa amefariki akiwa na miaka 24.

Madaktari walisema mwaka jana kuwa mwanafunzi huyo wa mwaka wa tatu alikuwa na maradhi ya moyo na figo kutokana na miaka mitano aliyokuwa akila chakula kidogo sana.

Maisha ya Wu Huayan yalikuwaje?

Wu Huayan na kaka yake waliishi katika mazingira magumu kwa miaka mingi baada ya kufiwa na wazazi wao wakiwa wadogo.

Yeye na ndugu yake walilelelwa na nyanya na baadaye mjomba na shangazi ambao waliweza kuwapatia yeni 300 kila mwezi.

Sehemu kubwa ya fedha hizo zilitumika kulipa malipo ya matibabu ya ndugu yake mdogo ambaye alikuwa anakabiliwa na changamoto za kiafya.

Hii ilimaanisha Bi Wu alitumia yeni mbili kwa siku ambayo ilimwezesha kununua mchele na pilipili kwa miaka mitano.

Alipowasili hospitali alikuwa na na urefu wa futi nne na nusu (4ft 5in).

Madaktari walisema alikuwa katika hali mbaya kutokana na ukosefu wa lishe kiasi cha kupoteza 50% ya nywele zake kichwani.

Kisa hicho kimepokelewaje?

Ndugu hao ambao wanatokea mkoa wa Guizhou, moja ya mikoa maskini zaidi nchini China na kisa hiki kimeeangazia hali mbaya ya umasikini nchini China.

Japo uchumi wa China umekuwa kwa miongo kadhaa iliyopita viwango vya umaskini havijapungua, huku takwimu ya kitaifa ya mwaka 2017 zikionyesha kuwa takribani watu milioni 30.46 wanaoishi katika maeneo ya mashambani wanaishi chini ya dola $1.90 kwa siku.

Viwango vya ukosefu wa usawa pia viliongezeka huku ripoti ya mwaka 2018 ya shirika la fedha duniani, IMF, ikisema kuwa China ni ''moja ya mataifa yasiyokuwa na usawa duniani''

Kisa cha Wu Huayan kilizua ghadhabu kwa umma dhidi ya mamlaka katika mitandao ya kijamii huku baadhi ya watu katika mitandao ya kijamiii wakisema ndugu hao walitelekezwa.

Wengine walisifia upendo wake kwa kaka yake kiasi cha kujinyima vitu muhimu maishani mwake.

Kando na michango ya umma ilianzishwa kupitia mitandao ya kijamii walimu na wanafunzi wenzake walimchangia yeni 40,000, huku wanakijiji wakichanga yeni 30,000 kumsaidia.

Kabla ya kifo chake , maafisa walitoa taarifa kusema kuwa Bi Wu amekuwa akipokea msaada wa serikali kwa jamii - ambayo inasadikiwa kuwa kati ya yeni 300, 700 kwa mwezi - na kwamba sasa anapokea usaidizi wakati wa dharura ya yeni 20,000.
Chanzo- BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com