Na Amiri Kilagalila-Njombe
Jeshi la polisi mkoa wa Njombe limesema kwa nyakati tofauti watoto wanne mkoani humo wamepoteza maisha kutokana na maji.
Akizungumza na vyombo vya habari mkoani humo kamanda wa polisi Hamis Issa amesema,mtoto wa kwanza aliyefahamika kwa majina ya Alpha Pilla (6) mkazi wa mtaa wa Kibendange mjini Makambako na mwanafunzi wa shule ya Makoga akiwa akicheza 25-12-2019 alitumbukia kwenye dimbwi la maji yaliyotuama ambayo hutumika kwa shughuli za uchimbaji mchanga na kusababisha kifo chake.
Kamanda amesema tukio jingine ni la mtoto Shani Belevete (8) huko kijiji cha Msimbazi kata ya uhambule wilaya ya Wanging’ombe alikutwa ametumbukia ndani ya kisima cha maji na mpaka watu kutafuta ngazi alikutwa amekwishafariki.
Amesema tukio jingine linahusisha vifo vya watoto wawili Joel Kutika (6) na Abromovich Hosea (3) huko kijiji cha Saja wilayani Wanging’ombe mnamo tarehe 1-1-2020 walikufa maji katika mto Bokelo uliopo kijijini hapo huku kiini cha tukio hilo kikiwa ni wazazi kutokuwa makini na watoto wao wanapokuwa wanacheza.
Aidha kamanda wa polisi ametoa wito kwa wazazi kuwa makini na watoto huku jeshi hilo likianza kuchukuwa hatua kwa mzazi yeyote asiyekuwa makini kuhakikisha ulinzi wa watoto na kusababisha vifo vya uzembe.
Social Plugin