WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mradi wa ujenzi wa hoteli ya Golden Tulip Airport Zanzibar ni muhimu katika kuimarisha sekta ya utalii na huduma za malazi kwa wageni wanaotumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.
Amesema mradi huo unakwenda sambamba na juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuimarisha uwanja wake wa ndege ili kuongeza uwezo wake katika kutoa huduma bora kwa abiria na wafanyakazi wa mashirika ya ndege ya ndani na nje ya nchi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Januari 4, 2020), wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa hoteli hiyo. Miongoni mwa watakaonufaika na mradi huo ni pamoja na wasafiri wanaopita Zanzibar kwa ajili ya kuunganisha ndege na baadaye kuendelea na safari.
Waziri Mkuu ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hoteli ya Golden Tulip Airport Zanzibar inayojengwa katika eneo la uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya miaka 56 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yam waka 1964.
Ujenzi wa hoteli hiyo unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani milioni 8.5. sawa na sh. bilioni 19.55. “Ama kwa hakika uwekezaji huu ni mkubwa na naamini wawekezaji hawa wengeliamua kuwekeza katika nchi nyingine yoyote, nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wangelipokelewa kwa mikono miwili.”
“Hata hivyo, mazingira mazuri ya uwekezaji hapa Zanzibar na uzalendo alionao Mhe. Mohamed Raza, Mwenyekiti wa ‘Royal suites group of companies’ vilipelekea ushawishi mkubwa wa hoteli ya aina hii kujengwa hapa Zanzibar.”
Waziri Mkuu amesema kuwa “Nyote mtakubaliana nami kuwa viwanja vingi vya ndege vilivyopo kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki, havina hoteli kubwa na za kisasa zilizopo karibu na viwanja hivyo. Uamuzi wa kujenga mradi huu ni sahihi, kwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ni mahali salama na wezeshi kwa biashara na uwekezaji.”
Amesema kwa upande mwingine, Serikali zinaendelea kuimarisha amani na utulivu, miundombinu wezeshi ya kiuchumi, huduma za fedha na mifumo ya kodi ili kuvutia uwekezaji. “Mambo haya ni muhimu sana katika kuvutia wawekezaji katika sekta mbalimbali kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Hivyo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa pongezi za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein kwa juhudi wanazoendelea kuzifanya za kushajiisha uwekezaji. “Tunawashukuru sana.”
Amesema kwa upande wa Zanzibar, katika kipindi hiki cha miaka tisa ya Awamu ya Saba, ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, jumla ya miradi ya uwekezaji 304 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.74 imeidhinishwa na mingine iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Utekelezwaji wa miradi hiyo, umetoa mchango mkubwa katika kukuza ajira, teknolojia, kuongeza mapato ya Serikali na kuimarisha ustawi wa Wananchi wetu. “Hivyo, nawapongeza wawekezaji wetu wote waliowekeza na wanaoendelea kuwekeza hapa nchini. Wawekezaji hawa wameonesha imani na upendo mkubwa kwetu, nasi tunaahidi kufanya nao kazi kwa ushirikiano makubwa.”
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Mohammed Ramia amesema mradi huo ni muhimu kwa kuwa utakapokamilika utaenda kuongeza mapato ya Serikali.
Amesema hoteli hiyo ni ya kwanza kwa Zanzibar kwa sababu mbali ya kuwa na ukumbi wa watu mashuhuri (VIP Business Lounge) ambao wageni wake watakuwa na uwezo wa kukamilisha taratibu za abiria wa ndege (check in) na taratibu za uhamiaji moja kwa moja kutoka katika ukumbi huo.
Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa Royal Group of Companies, Bw. Hassan Mohammed Raza alisema ujenzi wa hoteli hiyo yenye vyumba 61, kumbi tatu za mikutano zenye uwezo uwezo wa kuchukua watu 600 ina hadhi ya nyota nne, ulianza februari 2019 na unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu.
Alisema nembo ya Golden Tulip ni sehemu moja ya kampuni ya pili kwa ukubwa duniani kwa upande wa hoteli ukiwa chini ya mwavuli wa Louvre Hoteli ambayo inamilikiwa na Shanghai Municipal Council. Mtandao huo una hoteli zaidi ya 8,000 duniani, hivyo hoteli yao italazimika kufuata na kutimiza vigezo bora vya hoteli katika sekta ya hoteli duniani.
(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
Social Plugin