WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli itaendelea kukemea utendendaji usioridhisha pale inapoona mambo hayaendi sawa katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na Zanzibar.
Amesema maagizo aliyoyatoa Jumamosi, Januari 18, 2020, wakati alipotembelea kiwanda cha kuzalisha sukari cha Zanzibar kilichopo Mahonda, wilaya ya Kaskazini ‘A’, mkoa wa Kaskazini Unguja ni sahihi kwa kuwa yanalenga kuboresha maendeleo na kulinda wawekezaji.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Januari 30, 2020) wakati akijibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashimu Ayoub (BLW) katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu. Mbunge huyo alitaka kufahamu ni lini Serikali itaruhusu sukari inayozalishwa na kiwanda cha Sukari Zanzibar iuzwe Tanzania Bara.
Amesema alipofanya ziara katika kiwanda hicho, alikuta tani 3,200 zikiwa hazijanunuliwa. “Nilipofika kiwandani hapo nilikuta sukari nyingi kwenye bohari kwa madai kuwa imekosa soko. Ingawa mbunge amesema anahitaji soko la Tanzania Bara lakini mahitaji ya sukari Zanzibar ni tani 36,000 kwa mwaka na kiwanda kinazalisha 6,000.”
Waziri Mkuu amesema mpango wa uagizaji sukari kutoka nje ya nchi hauko sahihi kwani wanunuzi walitakiwa kwanza wanunue sukari inayozalishwa ndani ndipo waagize nje kiasi kinachopungua.“Haiwezekani sukari inayozalishwa ndani ikakosa soko kutokana na uingizwaji wa sukari kutoka nje. Hii inawavunja moyo wawekezaji wetu,” amesema.
Hivyo, amesema yeye na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ndio wenye jukumu la kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM na kwamba suala la viwanda limo katika utekelezaji wa ilani hiyo.
“Ninapokuta Ilani haitekelezeki popote pale nchini lazima niwe mchungu, lazima tuweke mpango wa kuwalinda wawekezaji wa ndani na kuwahakikishia masoko na tunajua masoko hayo tunayo,” amesema.
“Pale wapo waagizaji wa sukari watatu tu, sasa kwanini wasipewe masharti rahisi ya kuanza kununua sukari ya ndani na kiasi kinachopungua ndio waagize. Lazima tulinde viwanda vyetu… halafu mtu anasema nimewachefua Wazanzibari. Hivi nimewachefua Wazanzibari ama nimewachefua wanunuzi?” amehoji.
Amesema sera ya nchi inasisitiza umuhimu wa kulinda wazalishaji wa ndani ambao bidhaa zao zimethibitishwa na mamlaka husika. Hivyo, ni lazima kuwalinda wawekezaji kwa kuhakikisha wanapata masoko ya uhakika.
Waziri Mkuu amesema viwanda vinasaidia katika kuondoa tatizo la ajira, vinawapa wakulima soko la uhakika la mazao yao pamoja na Serikali kupata kodi ya uhakika. “Kiwanda kile kimeajiri watu 400 na Serikali inapata kodi zinazowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.”
Amesema: “Mwekezaji asipozalisha, wale wananchi hawana ajira. Asipozalisha, atakosa mishahara ya kuwalipa wafanyakazi wake. Atashindwa kulipa kodi. Kutokana na kodi hizi, tumeona maabara inajengwa Bwejuu na kituo cha mama na mtoto pale Bambi; hivyo tutakuwa wakali pale ambapo mambo hayaendi.”
(mwisho)