Waziri mkuu wa Urusi Dmitry Medvedev ametangaza kujiuzulu hii leo 15.01.2020 akisema kuwa yeye pamoja na serikali anayoiongoza inaachia ngazi ili kumpa nafasi Rais Vladmir Putin kufanya mabadiliko ya katiba.
Medvedev ametoa tamko la kujiuzulu kupitia Televisheni ya Taifa ya Urusi akiwa ameketi sambamba na Rais Putin ambaye ni mshirika wake wa karibu. Kwa mujibu wa shirika la habari la Urusi, Putin amemshukuru waziri mkuu huyo aliyejiuzulu kwa utumishi wake huku akibainisha kuwa baraza lake la Mawaziri lilishindwa kutimiza majukumu yake.
Medvedev ametumikia wadhifa huo wa uwaziri mkuu wa Urusi tangu mwaka 2012, kabla ya hapo alikuwa Rais wa nchi hiyo toka mwaka 2008 hadi 2012. Baada ya kujiuzulu kwa Medvedev na mawaziri wake Rais Putin ameliomba baraza hilo la mawaziri kuendelea kufanya kazi hadi hapo baraza jipya litakapotangazwa.
Tangazo la waziri mkuu wa Urusi ambalo halikutarajiwa limetolewa muda mfupi baada ya Rais Putin kutoa hotuba mapema leo akipendekeza kura ya maoni juu ya mabadiliko kadhaa kwenye katiba ya nchi yake, yatakayolipa bunge nguvu zaidi
Social Plugin