Na Felix Mwagara, MOHA, Dodoma.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amewataka Watendaji Wakuu wa Wizara yake kufanya kazi kwa ushirikiano kwa kuwa Wizara hiyo ina mambo mengi yayonahusiana na jamii.
Akizungumza katika ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo jijini Dodoma, leo, Simbachawene amewataka watendaji hao wakati anajiandaa kuja mbele yao kuonyesha mbinu zake, wafanye kazi usiku na mchana, yale yanayohitaji kufanyiwa kazi yaweze kufanyiwa kazi.
“Lazima tufanye kazi usiku na mchana, lazima nchi yetu izidi kusonga mbele, na sasa hivi katika Afrika tunaonekana watu ambao tunajenga nchi kwa kasi, heshima hii aliyoileta mheshishiwa rais lazima sisi tuwe mashabiki wake,” alisema Simbachawene.
Pia Waziri Simbachawene alimshukuru Lugola kwa kumkabidhi ofisi hiyo na kumuahidi kuyatendea kazi yale yote mema aliyoyaacha.
“Yale maeneo uliyoyagusia na mazuri uliyoyafanya tutaendelea kuyaendeleza kwasababu yamesemwa katika ila ya chama cha mapinduzi na pia yapo katika mipango tutaendelea kuyaendeleza,” alisema Simbachawene.
Kwa upande wake Lugola, alisema Waziri hiyo aliwashukuru watendaji wa Wizara hiyo kwa kumpa ushirikiano katika kipindi chote cha uongozi wake, na kuwataka waendelee kufanya kazi kwa bidii ili kumsaidia Rais John Magufuli.
Pia alimpongeza Waziri Simbachawene kwa kuteuliwa kuiongoza Wizara hiyo, na Rais Magufuli amemwamini na hakubahatisha kumteua katika nafasi hiyo kutokana na uwezo na umahiri alionao.
“Ninachokifanya hapa utamaduni ambao hata mimi nilipoteuliwa nilikabidhiwa kutoka kwa mwenzangu, hivyo ni jambo la msingi tulilolifanya, na ninakupongeza san ana ninakuahidi kukupa ushirikiano kipindi chote
utakaponihitaji,” alisema Lugola.
Lugola aliongeza kuwa, Wizara hiyo inachangamoto nyingi zikiwemo za uhaba wa rasilimali watu kwa vyombo vya ulinzi na usalam, pamoja na changamoto ya ukosefu ya majengo ya kutolea huduma Mikoani na Wilayani.
“Pia kunachangamoto za vitendea kazi kama magari na vifaa vingine, pia kuna changamoto ya mafunzo ya kuwanoa rasilimaliwatu, pia Wizara inakabiliwa na changamoto ya rasilimali fedha, lakini licha ya kuwepo kwa changamoto hizo lakini hatujakata tamaa, tulifanya kazi kwa weledi,” alisema Lugola.
Makabidhiano hayo yalifanyika kuanzia saa 5:34 asubuhi na kumalizika saa 6:44 mchana, na kuhudhuriwa na viongozi wa Wizara pamoja na Taasisi zote za Wizara hiyo.
Social Plugin