Na Salvatory Ntandu - Malunde 1 blog
Wakazi watatu wa mtaa wa Nyahanga wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamefikishwa katika mahakama ya wilaya Kahama kwa tuhuma za kuvunja chumba cha kuhifadhia bidhaa (Store) na kuiba mali mbalimbali zenye thamani ya shilingi milioni tatu laki moja na elfu 46 mali ya Joyce Godlizen.
Waliofikishwa Mahakamani hapo ni pamoja na Ibrahimu Musa Matanyanga (26) Abdala Lucas (25) na Musa Daniel ambao kwa pamoja wanatuhumiwa kuvunja chumba hicho na kuiba mali hizo huku wakijua wazi kuwa kufanya hivyo ni kosa.
Akisoma shauri hilo Januari 28,2020 Mbele ya hakimu Mkazi mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Kahama Evodia Kyaruzi mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi, Shabani Mateso amedai kuwa watuhumiwa hao walitenda makosa hayo Januari 19 mwaka huu majira ya saa sita usiku katika mtaa wa Nyahanga.
Mateso alisema kuwa katika shauri hilo la Jinai namba 40 la mwaka huu watuhumiwa hao watatu wanakabiliwa na mashitaka mawili ambapo katika shitaka la kwanza la kuvunja chumba wamekiuka kifungu namba 267 cha kanuni ya adhabu sura 16 marejeo ya mwaka 2002.
Shitaka la pili la kuiba watuhumiwa hao wanadaiwa kuiba,Televisheni mmoja,godoro,sabufa,mchele kilo 40,mabegi mawili,shuka 15,vitenge 12,nguo mbalimbali,mafuta ya kula na fedha tasilimu laki tano na elfu sabini na sita kinyume na kifungu namba 258 na 265 cha kanuni ya adhabu sura 16 marejeo ya mwaka 2002.
Watuhumiwa hao walikana kutenda makosa yanayowakabili Mahakamani hapo na shauri hilo limeahirishwa hadi Febuari 11 mwaka huu ambapo litaendelea kusikilizwa.
Wote kwa pamoja wamerudishwa gerezani baada ya kushindwa kutimiza Masharti ya dhamani yaliyotolewa na Mahakama hiyo ya kuwa na wadhamini wawili wawili kila mmoja.
Social Plugin