Na Lulu Mussa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Azzan Zungu amemtaka kila mtumishi katika Ofisi ya Makamu wa Rais atimize wajibu wake katika kuleta maendeleo ya Taifa letu.
Hayo ameyasema hii leo mara baada ya kuwasili rasmi katika Ofisi ya Makamu wa Rais katika Mji wa Serikali Mtumba Dodoma na kupokewa na Menejimenti na watumishi na Ofisi hiyo.
Akizungumza na watumishi wa Ofisi yake Waziri Zungu amewataka wote kufanya kazi kwa ushirikiano na kuahidi kuendelea kusimamia Sheria, Taratibu na Kanuni zilizopo.
Ametoa rai kwa watanzania kuwa chachu ya mabadiliko katika kuhifadhi na kusimamia Mazingira. “Simamieni Sheria bila kumuonea mtu, pale ambapo Sheria imekataza jambo simamieni Sheria na kuchukua hatua kwa wote wanaokiuka” Zungu alisisitiza.
Awali aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ambae sasa ni wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene amekabidhi Ofisi rasmi kwa Waziri Zungu na kumtakia kila la heri katika kutekeleza majukumu yake mapya.
“Tumefanikiwa katika katazo la mifuko ya plastiki, tumeridhia Mikataba na Itifaki mbalimbali na pia tuna program maalumu ya Upandaji mti nchi nzima ambayo ni endelevu” Simbachawene alisisitiza.
Pia Mhe. Waziri Simbachawene alisema kuwa mbali ya kufanikiwa katika kampeni ya katazo la mifuko ya plastiki lakini zaidi na elimu inapaswa kutolewa kwa wananchi kuhusu tofauti ya vifungushio na vibebeo ambavyo bado wananchi wanachanganya.
Amempongeza na kumshukuru Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Mhandisi Joseph Malongo kwa muda aliofanya nae kazi kwa ukaribu ambapo wameweza kutekeleza majukumu mbalimbali yakiwemo kuridhia mikataba, itifaki na kanuni zinazohusu mazingira.
Waziri Zungu ameteuliwa hivi karibuni na Rais Dkt. John Magufuli kushika nafasi hiyo baada ya kufanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri ambapo Mhe. Simbachawene aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.