Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ameagiza kurejeshwa nchini humo raia 132 wa Taifa hilo waliopo kwenye mji wa Wuhan nchini China, mji ambapo virusi vya corona vimeanzia.
Rais Ramaphosa ametoa agizo hilo baada ya kikao cha Baraza la Mawaziri nchini Afrika Kusini, kikao kilichofanyika kutokana na familia nyingi nchini humo zenye ndugu zao katika mji wa Wuhan kuomba ndugu zao wasaidiwe kurejea nchini humo.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Afrika Kusini imeeleza kuwa, ratiba kamili ya kurejeshwa kwa raia hao bado haijapangwa, lakini watakaorejeshwa nyumbani ni 132 kati ya 199 waliopo katika mji huo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, raia hao wote wanaotaka kurejea nyumbani hawajaambukizwa virusi hivyo vya corona na wala hawajaonyesha dalili zozote za kupata homa hiyo, lakini watakapofika Afrika Kusini watawekwa kwenye karantini kwa muda wa siku 21 ndipo waruhusiwe kwenda katika maeneo yao.
Serikali ya Afrika Kusini imeandaa Wataalam wa afya wa kutosha pamoja na askari ambao watahusika na zoezi lote la kuwarejesha raia wake wanaoishi Wuhan na kuwahudumia kwa wakati wote watakapokua kwenye Karantini.
Tayari Shirika la Ndege la Afrika Kusini limefuta safari zake za moja kwa moja kutoka nchini humo kwenda China.