Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo ameonya mipango ya serikali ya Afrika Kusini kunyakua ardhi pasipo fidia kuwa ''utaleta madhara mabaya sana'' kwa uchumi na taifa kwa ujumla.
Pompeo alitoa kauli hiyo nchini Ethiopia, alipofanya ziara Afrika, ambapo pia alifanya ziara Angola na Senegal.
''Afrika Kusini iko kwenye mjadala wa kufanya mabadiliko ya sheria kuhusu kuchukua mali binafsi bila kulipa fidia. Suala hilo ni hatari kwa uchumi lakini lakini pia kwa watu wa Afrika Kusini,'' alinukuliwa na shirika la habari la Bloomberg.
Uchumi wa Afrika ulihitaji ''Utawala wa sheria wenye nguvu, heshima kwa haki ya umiliki na sheria zinazochochea uwekezaji''. aliongeza.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ameapa kuharakisha mchakato wa marekebisho kwenye kifungu cha katiba kuhusu unyakuaji ardhi bila fidia ili kurejesha haki ''iliyopokwa miaka ya nyuma'' iliyosababishwa na utawala wa watu weupe wachache.
Mashamba mengi yanamilikiwa na wakulima wa kizungu kwa 72% kwa mujibu wa takwimu za serikali. na jamii hiyo ya watu weupe ni 9% ya raia wa Afrika Kusini.
Mipango ya serikali ilikuwa ikipingwa vikali na chama kikuu cha upinzani Democratic Alliance, na hasa makundi ya jamii ya watu weupe wenye ushawishi.
Mwaka 2018, Rais wa Marekani Donald Trump alimtaka bwana Pompeo ''kufuatilia kwa karibu vitendo vya kuzuia na kunyakua ardhi na mashamba na mauaji ya wakulima wakubwa.''
Serikali ya Afrika Kusini imesema Trump ''amepotoshwa'' na kuwa suala hilo litashughulikiwa kwa kupitia mifumo ya kidiplomasia.
-BBC
Social Plugin