Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

POLISI MOROGORO WAKAMATA GARI LILILOBADILISHWA NAMBA YA USAJILI LIKISAFIRISHA BANGI

Na Jackline Lolah - Morogoro
Jeshi la polisi mkoani Morogoro limefanikiwa kukamata watuhumiwa 9 wa makosa mbalimbali ikiwemo bangi magunia 8 madumu mawili ya ujazo wa lita 20 yaliyojazwa bangi, gari moja aina ya prado na pikipiki zilizokuwa zinasafirisha bangi pamoja na dawa zidhaniwazo kuwa ni za kulevya aina heroine zenye ujazo wa gram 29.

Akizungumza na waandishi wa habari leo februari 21,2020 kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro ACP Mugabo Wekwe amesema kuwa askari wakiwa doria walipokea taarifa za kuwepo kwa gari lenye namba za usajili T. 612 DEM aina ya prado yenye rangi ya silva iliyokuwa ikiendeshwa na Jaffunery Jaji Emmanuel (24)mkazi wa mtaa wa Makoka Ilala jijini Dar es salaam na Modest Salim (30) Mkazi wa Kwamrombo Arusha likiwa limebeba bangi. 

"Baada ya kufanya upekuzi wa gari hilo askari waliwakuta wakiwa na bangi gunia 8 sawa na kilogram 150.17 zilizopakiwa kwenye gari hyo ambayo iliwekwa namba za DFP 5363 za bandia kwa lengo la kusafirisha bangi hiyo kwa urahisi bila kutiliwa mashaka ambapo bangi hiyo walikuwa wakisafirisha kutoka Dodoma kwenda Dar es salaam, hadi sasa watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa na hatua za kuwafikisha mahakamani zinafuata",amesema Kamanda  Wekwe.

Katika hatua nyingine amesema mnamo tarehe 20/2/2020 majira ya saa nne asubuhi huko maeneo ya Green barabara kuu ya Morogoro - Iringa kata na tarafa ya Mikumi wilaya ya Kipolisi Ruhembe jeshi la polisi mkoani Morogoro limefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu watano raia wa Ethiopia wakiwa hawana passport. 


"Wahamiaji hao ni Mulken Tesfaye (28), Samuel Wamebo (21), Mohamed Amani (23), Abdilsalmin Amsnr (20) pamoja na Solomon Demekwe (20) ambapo wawili kati yao walifungiwa kwenye buti nyuma ya gari na watatu walilala kwenye kiti cha dereva, watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa na hatua za kuwafikisha mahakaman zinafuata",amesema. 

Hivyo jeshi la polisi linaendelea kutoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi pindi wanapo kutana na uhalifu na wahalifu wa aina zote. 

"Pia niwatake wale wote wanao jaribu kufanya biashara haramu za kusafirisha na kusambaza bangi na dawa za kulevya za viwandani waache mara moja kwani jeshi la polisi limejipanga vizuri kuhakikisha linawatia mbaroni na kuwafikisha mahakamani",ameongeza Kamanda. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com