Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuwa kinara katika kuisaidia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kukusanya mapato katika sekta ya Utalii. Mwaka jana Benki ya CRDB kupitia mifumo yake ya kidijitali iliweza kukusanya kodi na tozo kwa watalii na wageni zinazofikia dola za kimarekani milioni 12 kutoka dola laki 4 mwaka 2014 ambapo ni ongezeko la takribani asilimia 3000.
Akizungumza katika Semina maalum iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa ajili ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na viongozi wengine wa taasisi za Serikali Mheshimiwa Zuberi Ali Maulid, alisema Benki ya CRDB imekuwa kiungo muhimu katika uchumi wa Zanzibar hususani katika kuweka miundo mbinu thabiti ya huduma za kifedha kwa Wazanzibari na wageni.
“Benki ya CRDB ni mshirika muhimu katika uchumi wa Zanzibar, hususan kipindi hiki tukiwa tunakwenda kukamilisha Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2020. Serikali inafurahishwa sana na namna ambavyo tumekuwa tukishirikiana na Benki hii katika kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea,” alisema Mhe. Zubeir Maulid.
Mheshimiwa Zubeir Maulid alisema moja ya mafanikio makubwa ambayo Serikali imeyapata kutokana na ushirikiano baina yake na Benki ya CRDB ni kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato ambao unatokana na uunganishwaji wa mifumo ya kidijitali ya malipo ya Benki ya CRDB. “Mwaka jana wametusaidia kukusanya zaidi ya dola za kimarekani milioni 12, hiki ni kiwango kikubwa sana ambacho kinatokana na ufanisi wa mifumo hii ya kidijitali ya Benki ya CRDB,” alisema Mhe. Zubeir Maulid.
Mhe. Zubeir Maulid alisema kuongezeka kwa ukusanyaji huo katika sekta ya utalii kunasaidia kuongeza kwa Pato la Taifa, na hivyo kuiongeza serikali uwezo katika utoaji wa huduma za kijamii. Pia alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafurahishwa na ushiriki wa Benki ya CRDB katika sekta nyengine za maendeleo ikiwamo kilimo, biashara na viwanda pamoja na ujenzi wa miundombinu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela alisema kwamba Benki ya CRDB imedhamiria kufanya kazi kwa karibu zaidi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufikia malengo ya kujenga nchi yenye uchumi wa kati kupitia uwezeshaji katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
"Tunafahamu Serikali imejipanga kuleta mapinduzi katika sekta zote za maendeleo na sisi tumeweka mikakati ya ushiriki wetu katika kuisaidia Serikali kuanzia sekta ya kilimo, utalii, ujenzi, uchakataji wa mazao na uwekezaji kwenye viwanda,” alisema Nsekela huku akibainisha kuwa benki hiyo pia imejipanga pia kuwezesha sekta binafsi ambayo ni mshirika wa maendeleo wa Serikali nchini.
Nsekela alisema usahili wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Tabianchi (GCF) ulioipata Benki hiyo mwishoni mwa mwaka jana umesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza uwezo wa benki hiyo kutoa mikopo ambapo sasa hivi inaweza kutoa hadi dola za kimarekani milioni 250 kwa mradi mmoja.
“Hizi ni fedha nyingi sana ambazo tumedhamiria kuzielekeza katika miradi ya maendeleo nchini kwa kushirikiana na Serikali na sekta binafsi,” aliongezea Nsekela.
Semina hiyo maalum kwa ajili ya Wajumbe na Baraza la Wawakilishi na Viongozi wa Serikali Zanzibar ambayo ilikuwa na kauli mbiu ya “Pamoja Kujenga Uchumi”, ililenga katika kujadiliana namna ya kuboresha ushirikiano kati ya Serikali na Benki ya CRDB katika kufanikisha miradi ya maendeleo nchini pamoja na kusogeza huduma za kibenki karibu zaidi na wananchi ili kuchochea ukuaji wa uchumi.