Msimu wa 17 wa Sauti za Busara umeanza rasmi leo Alhamis ya Februari 13 hadi 17 utakaofanyika eneo la kihistoria Ngome Kongwe likiwa na wadhamini mbalimbali ikiwemo Benki ya CRDB.
Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla iliyofanyika katika Hoteli ya Marumaru, Stone Town, Zanzibar mwakilishi wa Meneja wa Benki ya CRDB tawi la Zanzibar Ndugu Jerome Saraka ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Makusanyo ya VISA uwanya wa ndege amesema:
"Leo tunapotambulisha rasmi udhamini huu wa milioni 20, tunadhamiria kulenga mambo makubwa matatu, moja kuongeza nguvu katika kutangaza vivutio vya utalii vya nchi yetu katika tamasha hili la Sauti za Busara, mbili kushiriki katika juhudi za kufungua milango ya uwezeshaji kiuchumi kupitia watalii ambao watakuwa wakihudhuria katika tamasha hili la Sauti za Busara na tatu kushiriki katika juhudi za kutambulisha vipaji vya muziki na uigizaji ambavyo ni sehemu kubwa ya ajira kwa vijana wa taifa hili.
Kupitia kampeni yetu ya malipo kwa kadi ya “Scan, Chanja, Lipa Sepa,’ benki itaendelea kuwahamasisha wahudhuriaji wa tamasha la sauti za Busara kutobeba pesa taslimu, kwani wanaweza kufanya manununzi na malipo yao , kupitia mashine zetu za kulipia fedha popote ndani ya Zanzibar.
Aidha Benki ya CRDB pia itashiriki kikamilfu katika tamasha hili kwa kuweka gazebo la mauzo katika viwanja vya tamasha hilo. Gazebo hilo litatoa huduma ya kubadili fedha za kigeni na huduma za kuweka na kutoa fedha kupitia wakala. Benki ya CRDB pia imeandaa shindano maalumu litakalo wawezesha wateja wake kujishindia safari ya kuhudhuria tamasha hilo. Jumla ya nafasi nne zitatolewa.
Ambapo kila mshindi atapata nafasi ya kumleta na mwenza wake. Washindi wanapatikana kupitia ushiriki wao kupitia akaunti za Benki za mitandao ya kijamii.
Washindi wanne watalipiwa gharama zote kuanzia safari, malazi na chakula. Nawashauri wateja wetu kufuatilia taarifa za shindano hili kupitia kurasa zetu za mitandao ya kijamii ili kujua jinsi ya kushiriki na kushinda.
Social Plugin