Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu leo ametoa taarifa ya mwenendo juu ya mlipuko wa ugonjwa wa Homa kali ya Mapafu inayosababishwa na virusi vipya jamii ya Corona (COVID - 19) ikiwa ni muendelezo wa taarifa tunazotoa mara kwa mara wakati wa milipuko.
Katika Taarufa hiyo Waziri Ummy Mwalimu amesema Idadi ya wagonjwa duniani imeendelea kuongezeka ambapo hadi kufikia tarehe 27 Februari, 2020 jumla ya watu 83, 652 wamethibitika kuugua, na kati ya hao wagonjwa 2,858 wamefariki. Asilimia 94 ya wagonjwa waliothibitika duniani wapo nchini China. Hadi sasa jumla ya nchi 51 zimeripoti ugonjwa huu ambapo kati ya hizo tatu ni nchi za Afrika ambazo ni Algeria, Nigeria na Misri.
Awmewatoa wasiwasi wananchi kuwa hadi sasa Tanzania haina mshukiwa wala mgonjwa wa ugonjwa wa kirusi cha corona (COVID - 19). Hata hivyo, bado nasisitiza kuwa tunahitaji kuendelea kuchukua Tahadhari kubwa ya kujikinga kupata ugonjwa huu kutokana na kuwa na muingiliano wa wasafiri kati ya Tanzania na mataifa mengine yaliyoathirika.
Ameongeza katika taarifa hiyo kuwa Kutokana na hatari iliyopo ya maambukizi ya ugonjwa huu, Serikali imejiandaa kukabiliana na tishio la ugonjwa huu, hususan kupitia maandalizi ya muda mrefu ambayo tumekuwa tukiyafanya kukabiliana na magonjwa hatari ya kuambukiza. Hatua mbalimbali tayari zimechukuliwa, na zinaendelea kuchukuliwa ambazo ni pamoja na:
Kuendelea na uchunguzi na ufuatiliaji wa wasafiri wote wanaoingia nchini kwenye mipaka yetu ikiwemo viwanja vya ndege, bandari na mipaka ya nchi kavu.
Kwa kipindi cha kuanzia Januari 30 hadi 27 Februari mwaka huu, jumla ya wasafiri 11,048 wamechunguzwa katika mipaka yetu ambao wanatokea katika nchi zilizo na ugonjwa huu kwa sasa ikiwamo China.
Wizara inavyo vipima joto 140 (vya mkono 125 (hand-held thermo scanners) na vya kupima watu wengi kwa mpigo 15 (Walkthrough thermoscanners)) ambavyo vimefungwa na vinatumika katika maeneo yetu ya mipakani ikiwemo viwanja vya ndege na bandari.
Vilevile tumeongeza idadi ya wataalamu wa afya katika maeneo ya mipakani ikiwa ni pamoja na kuajiri watumishi 100 ili kuimarisha ufuatiliaji wa wasafiri wanaoingia nchini kupitia maeneo ya mipakani.
Tumeandaa dawa, vifaa kinga na vitakasa mikono (Alcohol-based sanitizers) ambavyo tayari vipo kwenye Bohari za Dawa za Kanda kwa ajili ya kutumika endapo kutatokea mgonjwa.
Tumeandaa maeneo maalum katika mikoa yenye uwezekano mkubwa wa kupata wagonjwa kwa ajili ya kuwaweka washukiwa na kuwapatia matibabu wagonjwa.
Serikali imeimarisha uwezo wa kupima sampuli kupitia Maabara yetu ya Taifa ya Afya ya Jamii kwa watu wote wanaohisiwa kuwa na viashiria au dalili za ugonjwa huu ambapo ndani ya masaa 4 – 6 tunaweza kutoa majibu ya vipimo.
Tumeendelea kutoa elimu ya afya kwa umma kupitia njia mbalimbali ili wananchi na watoa huduma waendelee kuchukua tahadhari.
Pia, tumetoa mafunzo kwa watumishi wa sekta ya afya katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko na majanga ikiwemo jinsi ya kutoa matibabu ya magonjwa ya milipuko, kuchukua sampuli, uelimishaji na kuzingatia kanuni za afya.
Wizara imeisha waelekeza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kubainisha vituo vya kutolea matibabu kwa washukiwa/wagonjwa wa covid-19 endapo watatokea ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba vituo hivi vina vifaa vyote muhimu vya kutolea huduma.
Ugonjwa huu huenezwa kwa njia ya majimaji yatokayo njia ya hewa wakati mtu mwenye ugonjwa huu anapokohoa au kupiga chafya, kugusa majimaji yanayotoka puani (kamasi), kugusa vitambaa au nguo zilizotumiwa na mtu aliyepata maambukizi ya ugonjwa huu au maeneo mengine yaliyoguswa na mtu mwenye virusi vya ugonjwa huu.
Hivyo ni muhimu kwa kila mwananchi kufanya yafuatayo ili kuzuia ugonjwa huu usiingie nchini:-
Kufuata kanuni za Afya kwa kufunika mdomo na pua wakati wa kukohoa kwa kitambaa safi au nguo uliyovaa sehemu za mikono (Kiwiko cha mkono kuzuia hewa/makohozi kusambaa na kuhatarisha wengine).
Kuzingatia usafi binafsi ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono.
Kujizua kupeana mikono na kukumbatiana.
Kuepuka kugusana na mgonjwa mwenye dalili za magonjwa ya njia ya hewa mwenye historia ya kusafiri maeneo au nchi zilizoathirika na ugonjwa huu.
Kuwahi kwenye kituo cha kutolea huduma za afya endapo utakuwa na dalili za ugonjwa huu.
Kutoa taarifa ya uwepo wa mtu mwenye dalili
zinazohiswa kuwa za ugonjwa huu kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu nawe au piga simu namba 0800110124 au 0800110125 bila malipo.
Kusubiri au kuepuka safari zisizo za lazima kwenda kwenye maeneo yaliyoathirika na inapolazimu kusafiri, wasafiri wanapaswa wapate maelezo ya kitaalamu kabla ya kuondoka nchini. Kwa wale ambao wanafanya biashara, tunashauri wafanye biashara mtandao katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa huu.
Aidha, Serikali inatoa maelekezo kwa Mikoa yote nchini kufanya yafuatayo:
Kuhakikisha ndani ya siku tatu wanawasilisha kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya jina la kituo ambacho kimetengwa maalum kwa ajili ya kuhudumia washukiwa au wagonjwa endapo watatokea katika kila Halmashauri.
Kuhakikisha Hospitali zote, za umma na binafsi, zilizoko katika maeneo yao zina eneo la muda la kumshikilia mshukiwa.
Kuimarisha uzingatiwaji wa Kanuni za kuzuia maambukizi (Infection Prevention and Control- IPC) kwa kuhakikisha watumishi wanahimizwa na wanapatiwa vifaa vinavyohitajika.
Aidha, Mikoa ihakikishe uwepo wa vitakasa mikono katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu ikiwemo mahoteli, nyumba za wageni, sehemu za ibada, shule, ofisi, sehemu za kazi na biashara
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kufanya mawasiliano kwa karibu na serikali ya China kuhusiana na watanzania 504 ikiwepo Wanafunzi waliopo mji wa Wuhan. Ninapenda kuwaondoa wasiwasi kuwa watanzania hawa wapo kwenye mikono salama. Hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa kuhakikisha wako salama na mahitaji yao muhimu wanapatiwa.
Akihitimisha taarifa hiyo ameendelea kusisitiza kuwa ushirikiano wa pamoja wa wananchi, sekta na wadau mbalimbali katika kuzuia na kukabiliana na mlipuko huu ni muhimu. Hii ni pamoja na wananchi kuendelea kuwa wavumilivu kipindi hiki ambacho bado ugonjwa huu haujadhibitiwa na unaendelea kusambaa katika mataifa mengi.
Amesema serikali inaendelea kufuatilia kwa umakini mkubwa hali ilivyo duniani na endapo itatengamaa tutawajulisha haraka. Nitoe rai kwa wananchi kutosambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa na mamlaka husika.
Akimalizia kutoa taarifa hiyo amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya, likiwemo shirika la Afya Duniani (WHO) na sekta ya habari katika kuhakikisha kuwa afya za wananchi zinalindwa na elimu ya kutosha inatolewa.