Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DKT NCHIMBI AWATWISHA MZIGO TBS NA SIDO



 Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi

Na John Mapepele


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amelielekeza Shirika  la  Viwango nchini (TBS) na Shirika la Viwanda Vidogo nchini (SIDO) kuanzisha mara moja  operesheni maalum ya  kuwatafuta wamiliki wa viwanda  na wazalishaji wakubwa wa mafuta ya alizeti katika Mkoa wa Singida.

Lengo kubwa ni kukagua viwango vya  mafuta  hayo na kuwaelimisha  ili  kuhakikisha ubora wa mafuta hayo yaweze  kuingia kwenye  masoko ya kimataifa hatimaye kuinua  uchumi wa  mwananchi mmoja mmoja  na taifa kwa ujumla.


Dkt. Nchimbi ametoa maelekezo hayo kwenye mafunzo maalum ya kudhibiti ubora wa bidhaa yaliyotolewa na TBS kwa wajasiliamali  wa zao la alizeti  na asali yaliyofanyika katika ukumbi wa VETA  hivi karibuni.

Ambapo pia amelipongeza TBS na SIDO kwa kubuni utaratibu wa kutoa mafunzo  hayo  nchi nzima  huku akiwataka kwenda mbali zaidi  kwa kuwa karibu na  kufanya tathmini ya mara kwa mara  kwa mafunzo wanayoyatoa kwa wajasiliamali na kuchukua hatua stahiki.




Amesema  katika dunia ya sasa suala la kuzingatia viwango katika  bidhaa zote hususan   bidhaa za vyakula kwa binadamu la lazima na la kisheria  hivyo  mafunzo  yanayotolewa na TBS na SIDO lazima  yawaguse wahusika ili mafunzo hayo yawe na tija  badala ya kuendelea kutoa mafunzo hayo kwa mazoea.


“Inapofika  suala la  viwango  na ubora wa mafuta yetu  ya alizeti kwenye Mkoa wetu wa Singida linakuwa siyo suala la kubembelezana tena ili kinachozalishwa  kufika salama kwa mlaji” alisisitiza Mkuu wa Mkoa


Amewataka  wazalishaji na wamiliki wa viwanda vya alizeti na asali kuondokana  na fikra potofu za  kuona kuwa TBS ni adui badala yake kujenga ushirikiano wa karibu  ili kuhakikisha kuwa wananufaika  na huduma zinazotolewa na  hatimaye kuboresha  bidhaa wanazozizalisha  na kupata ushindani kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.


Aidha  amesema TBS ni daraja   baina ya mzalishaji, soko na mlaji  na kuwataka  wajasilia mali  kuwa  karibu ili kutengeneza fursa za biashara zao.


Amesema  tafiti nyingi zimeonesha kuwa  magonjwa mengi ya binadamu yanatokana  na  vyakula   tunavyokula hivyo udhibiti wa ubora  ni jambo lisilokwepeka  kwa sasa ili kunusuru vifo ambavyo vingeweza kuepukika.


Akitolea mfano katika kitabu kitakatifu  cha Mungu  cha Biblia amesema  maandiko  yanasema  hata kabla  ya kumuumba binabamu  Mwenyezi Mungu  alimtengenezea   chakula na pia  kinasisitiza kuwa mtu asiyefanya kazi na asile hivyo ni muhimu kuangalia chakula tunachokula  kwa afya ya mlaji.


Aliongeza kuwa  vitabu vyote vitakatifu  hakuna sehemu yoyote vinaposema mfanyabiashara awe  muongo akawataka  wasifanye  mchezo  na maisha ya  binadamu  kwa kukiuka  viwango  ili kupata  faida  ambapo alisisitiza  kwamba baada ya masomo hayo wajasiliamali wote watoke na viapo  vya moyoni vya kutenda haki na kuwa na hofu ya Mungu katika  utekelezaji wa biashara zao.


Amesema  Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli imedhamilia kwenda kwenye safari ya uchumi wa kati wa viwanda  kwa kuwashirikisha  wajasiliamali wote hapa nchini  hivyo kila mjasiliamali ana haki sawa  kwenye  safari  hii ambayo imeshatoa mafanikio makubwa.


 Naye  Mwalimu Hamis Sudi ambaye  ni Kaimu Mkurugenzi wa udhibiti ubora amemshukuru Mkuu wa Mkoa  na kumhakikishia  usimamizi shirikishi kwenye  udhibiti wa ubora kwenye  bidhaa zinazotokana na zao la alizeti katika mkoa wa Singida na kwamba operesheni maalum itafanyika ili kuwafikia  watengenezaji na wamiliki wa viwanda vya alizeti badala ya kutoa  mafunzo kwa wajasiliamali waliofika kuhudhulia mafunzo hayo.



“Mkuu wa Mkoa naomba  nikuhakikishie  hatujafika hapa Singida kupoteza  fedha na muda wa Serikali bali  kuwafikia wadau wetu wote ambao tutawafikia na tutaleta taarifa ya  utekelezaji katika ofisi yako” aliongeza Sudi.


Mkuu wa Idara ya Uhusiano wa TBS, Rhoida Andusamile amesema Shirika lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge – Sheria ya Viwango Na.3 ya mwaka 1975,iliyofanyiwa marekebisho na Sheria Na. 1 ya mwaka 1977.Sheria  hiyo ilifutwa na nafasi yake kuchukuliwa na Sheria ya Viwango Na.2 ya mwaka 2009 ambayo ililipa Shirika uwezo mkubwa zaidi wa kutekeleza majukumu yake.


Ameongeza kuwa Shirika lina majukumu mengi kama yalivyoainisha katika Sheria ya Viwango Na.2 ya mwaka 2009, lakini majukumu makuu manne.


Aliyataja mambo hayo ni kuweka viwango vya kitaifa vya bidhaa,huduma na mifumo ya usimamizi wa ubora katika sekta zote kutekeleza viwango vya kitaifa katika sekta za viwanda,biashara na huduma kwa kutumia skimu mbalimbali za udhibiti ubora.

Hata hivyo aliongeza kwamba pamoja na hayo lakini pia upimaji wa bidhaa kwa lengo la kuhakikisha ubora wake,pamoja na uthibitisho wa usahihi wa vipimo vinavyotumika viwandani na kutoa mafunzo kwa wazalishaji pamoja na wafanyakazi katika taasisi na viwanda kuhusiana na uzalishaji wa bidhaa bora,uzalishaji salama na usimamizi wa ubora.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com