Hatima ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, anayekabiliwa na kesi ya uchochezi itajulikana Aprili Mosi kama ana kesi ya kujibu au la.
Hatua hiyo imefikiwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi wao.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kuwa kesi hiyo imepangwa kwa ajili ya kusikilizwa, lakini upande wa Jamhuri umefunga ushahidi wao na kwamba mashahidi watatu wanatosha kujenga kesi yao.
Hakimu Simba alisema upande wa utetezi uwasilishe hoja zao ndani ya siku 14 na upande wa Jamhuri uwasilishe majibu baada ya siku 14 nyingine.
Alisema mahakama yake itatoa uamuzi wa kama Mdee ana kesi ya kujibu au la Aprili Mosi.
Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Julai 3, 2017 katika Makao Makuu ya Ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), iliyopo Mtaa wa Ufipa Wilaya ya Kinondoni, Mdee anadaiwa kutamka maneno dhidi ya Rais John Magufuli kuwa “anaongea ovyo ovyo, anatakiwa afungwe breki” kwamba kitendo ambacho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Social Plugin