Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HATIMA YA TUNDU LISSU KUHUSU UBUNGE WAKE KUJULIKANA KESHO

Mahakama Kuu kesho itaanza kusikiliza maombi ya aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, kumruhusu kwenda Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi wa Spika wa Bunge, Job Ndugai, kumvua nafasi ya ubunge wa jimbo hilo.


Juni 20, mwaka jana, Spika alitangaza kumvua Lissu ubunge kwa madai ya kutotimiza masharti ya kuendelea kuwa mshiriki katika shughuli za Bunge.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Msemaji wa familia ya Lissu, Wakili Alute Mughway, alisema Mahakama Kuu Masjala ya Dar es Saalam, Februari 25, mwaka huu, itasikiliza maombi ya Lissu, endapo atakubaliwa kwenda Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi wa kuvuliwa nafasi yake ya ubunge.

Mughway alisema, Lissu alipeleka ombi hilo Septemba mwaka jana dhidi ya Spika Ndugai kumvua nafasi yake ya ubunge na kutangaza Jimbo la Singida Mashariki kuwa wazi.

Septemba 9, 2019, Mahakama Kuu, ilitupilia mbali ombi la Lissu la kupinga kuvuliwa ubunge.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Sirilius Matupa, alisema maombi ya Lissu hayatekelezeki kwa sababu mleta maombi alitakiwa kufungua kesi ya kupinga uchaguzi mahakamani, badala yake alipeleka maombi ya kutaka kupinga uamuzi wa Spika.

Msemaji huyo wa familia, Mughway, alisema Lissu, hajaridhishwa na uamuzi wa Mahakama Kuu, hivyo amepeleka maombi mengine kuruhusiwa kwenda Mahakama ya Rufani kutolea uamuzi kama hukumu ya Jaji Matupa ni sahihi kisheria.

Alisema maombi hayo, kwa mara ya kwanza yalitajwa Desemba mwaka 2019, na Februari 25, mwaka huu yatakwenda kusikilizwa.

Akizungumzia Lissu kurejea nchini kutokana na kukamilisha matibabu yake, alisema atarudi baada ya muda kidogo, kwa kuwa anasubiri uchunguzi wa mwisho wa madaktari kuangalia kama matibabu aliyopewa yamekidhi viwango.

Licha ya kuzungumza hayo, alisema Lissu alikuwa na mpango wa kurejea nchini kuendelea na shughuli zake, lakini kinachomkwamisha ni kuhofia ulinzi na usalama wake.

Credit: Nipashe


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com