Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Wilayani Kahama inatarajiwa kukamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi zaidi ya laki 340 wa Halmashauri hiyo mwezi Aprili mwaka huu.
Akitoa maelezo hayo jana tarehe 10/02/2020 mbele ya Kamati ya siasa ya Mkoa wa Shinyanga iliyotembelea Hospitalini hapo na kukuta hatua za mwisho za ujenzi, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Michael Matomola amesema ujenzi wa Hospitali hiyo umegharimu sh. Bilioni 1.5 iliyotolewa na Serikali kuu.
Matomola amesema pia kuwa, Hosptali itaanza huduma kwa kutumia watumishi waliopo kwani vifaa tiba na dawa tayari vipo.
Aidha, Matomola ameongeza kuwa katika bajeti ya mwaka huu, Halmashauri imetenga kiasi cha sh. Milioni 500 kwa lengo la kuendeleza ujenzi ikiwemo jengo la kuhifadhia maiti.
Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi ikiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Bw. Mabala Mlolwa, ambayo ipo katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na Serikali Mkoani hapa, imetembelea na kukagua miradi mbalimbali kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu na Mji Kahama ikiwemo ujenzi wa barabara ya lami km 5 inayojengwa kwa sh. Bilioni 2.2 kata ya Nyamilangano, maeneo ya uwezeshaji wananchi kiuchumi Kahama Mji , ujenzi wa jengo la wagonjwa nje Hospitali ya Mji Kahama na ujenzi wa kituo cha Afya Nyasubi.
Wajumbe wa Kamati hiyo wamepongeza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Ilani na kusema kuwa Serikali imefanya kazi kubwa katika kuwahudumia wananchi.
Majengo ya Hospitali hiyo na Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Shinyanga wakiwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya maendeleo.
Social Plugin