Idadi ya vifo kutokana na mlipuko wa virusi vipya vya corona imeongezeka leo na kupindukia 1,016, wakati Shirika la Afya Ulimwenguni - WHO likionya kuwa watu walioambukizwa na hawajasafiri kwenda China huenda wakawasha moto mkubwa katika janga hilo.
Ongezeko la vifo limekuja baada ya Rais Xi Jinping kufanya ziara isiyo ya kawaida katika hospitali moja ya Beijing, akiwa amevaa vifaa vya kujikinga, na kushauriana na wahudumu wa afya na wagonjwa.
Timu ya mwanzo ya ujumbe wa kimataifa unaoongozwa na WHO imewasili China, wakati nchi hiyo ikipambana kudhibiti virusi hivyo vilivyoambukiza zaidi ya watu 42,000 na kusambaa hadi nchi 25.
Vifo vingine 108 vimeripotiwa leo. Serikali ya China imewazuwia mamilioni ya watu katika miji kadhaa.
Serikali kadhaa za kigeni zimepiga marufuku watu kuwasili kutoka China na mashirika makubwa ya ndege yamesitisha safari ili kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo.
Social Plugin