ITALIA YAAHIDI KUWEKEZA KATIKA HIFADHI YA MAZINGIRA


Na Lulu Mussa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Zungu amesema Serikali ya Tanzania iko tayari kuendeleza mashirikiano na Serikali ya Italia katika nyanja za Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira.  


Hayo ameyasema leo Jijini Dar es Salaam mara baada ya kufanya mazungumzo na Balozi wa Italia hapa nchini Mhe. Roberto Mengoni katika Ofisi ndogo ya Makamu wa Rais Mtaa wa Luthuli Jijini Dar es Salaam. 


Amesema suala la Mabadiliko ya Tabianchi ni changamoto kubwa duniani kwa hivi sasa na nchi zinazoendelea ndio waathirika wakubwa kutokana na uchafuzi wa mazingira unaofanywa na nchi zilizoendelea. 


Waziri Zungu ametoa wito kwa Serikali ya Italia kuendeleza mashirikiano katika nyanja za udhibiti wa taka na kujenga uwezo katika uzalishaji wa nishati mbadala ili kukabiliana na uharibufu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti kwa matumizi ya kuni na Mkaa. 


“Serikali ya Rais John Joseph Pombe Magufuli inatekeleza ujenzi wa mradi mkubwa wa kufua Umeme katika maporomoko ya Mto Rufiji kwa lengo la kuongeza nishati ya Umeme na kukuza sekta ya viwanda nchini” Zungu alisisitiza. 


Asema kukamilika kwa mradi wa kufua umeme wa Mwalimu Julius Nyerere utachochea jitihada za Serikali za kupambana na uharibifu wa mazingira utokanao na ukataji wa miti kwa matumizi ya nishati ya kupikia. Ameongeza kusema kuwa jitahada za dhati zinatakiwa kuwepo pia katika uzalishaji wa umeme wa nishati ya jua na upepo. 


Kwa upande wake Balozi wa Italia nchini Tanzania amesema kuwa nchi yake inalenga kutoa msukumo zaidi katika mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya Tabianchi, kuhimiza kilimo rafiki kwa mazingira, nishati mbadala na nishati jadidifu.  


Waziri Zungu amemuhakikishia Balozi Roberto ushirikiano wa dhati katika kupambana na uharibufu wa mazingira nchini ili kuhakikisha Tanzania inabaki salama kwa taifa la sasa na vizazi vijavyo.
 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post