Serikali ya Mkoa wa Katavi kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi kikosi cha 202 na 401 wamefanikiwa kukamata Bunduki 50 zikiwemo 13 za kivita na tatu zilizotengenezewa nchi za ulaya aina ya G3 kufutia masako uliofanywa kwa muda wa siku 21 katika Makazi ya wakimbizi ya Katumba na Mishamo humo.
Operesheni hiyo imefanyika ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa mwezi Oktoba mwaka jana wakati wa ziara yake Mkoani Katavi kwa uongozi wa Serikali ambapo aliwataka kuhakikisha wanawakamata watu wote ambao wanamiliki silaha kinyume cha sheria na wanaoingiza Silaha kutoka Nchi ya Burundi kwa ajili ya kufanyia ujambazi na uwindaji haramu wa wanyama pori
Akitoa taarifa ya operesheni hiyo inayojulikana kwa jina la Operesheni safisha Katumba 2020 mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi Juma Homera ,Mkuu wa Briged ya Magharibi Brigedia Jenerali Jacob Mkunda alisema kuwa katika operesheni hiyo walikamata bunduki 50.
Alifafanua kuwa katika bunduki hizo walizofanikiwa kuzikamata ni bunduki za kivita 13 aina ya SMG , Bunduki tatu aina ya G3, Raifo moja na Gobole 33.
Aidha wamekamata risasi 28 na mitego ya kukamatia wanyama 13
Brigedia Generali Mkunda alieleza kuwa katika msako huo wameweza kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa 17 ambao ni Raia wapya wa Tanzania wenye asili ya nchi ya Burundi katika ya watuhumiwa hao wanne wamekamatwa katika Makazi ya Wakimbizi ya Katumba Wilaya ya Mpanda na 14 wamekamatwa katika Makazi ya Wakimbizi ya Mishamo Wilaya ya Tanganyika
Alisema kuwa kwenye msako huu wameweza kubaini uwepo wa viwanda vya kutengeneza bunduki aina ya gobole kwenye makazi ya wakimbizi ya Mishamo ambazo zimekuwa zikitumika katika kufanyia ujangili wa kuua wanyama kwenye Hifadhi ya Taifa ya Katavi na kwenye mapori ya akiba .
Nae Mkuu wa oparesheni hiyo safisha Mishamo na Katumba Kanali Evance Mallaso alieleza kuwa wakazi wengi wanaoishi kwenye makazi hayo ya Katumba na Mishamo wamekuwa na tabia ya kuishi kwa usiri mkubwa wa kutowataja wahalifu wanaoingiza silaha kutoka nchi ya Burundi .
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Juma Homera alisema kuwa vyombo vya usalama katika Mkoa wa Katavi vimefanya kazi kubwa katika kufanikisha kukamatwa kwa silaha hizo
Amewaonya watanzania ambao wanaoishi kwenye makazi hayo ambao wamekuwa wakiwapokea wageni wanaoingiza silaha kutoka nchi za jirani kwa kuzificha kwenye ndoo na kwenye madumu wanapozisafirisha wanaofanya hivyo watambue kuwa na wao wakibainika watakamatwa tuu kwani Mkoa huu vyombo vya usalama vipo kazini muda wote .
Homera alieleza kuwa zoezi hilo la kuwasaka wanaomiliki silaha kinyume na sheria ni endelevu linaendelea hivyo hakuna mwalifu yoyote ambae ataweza kushindana na vyombo vya dola .
Alisema wakati wa ziara ya Rais Magufuli aliyoifanya oktoba 10 mwaka jana alisikitishwa sana na tabia ya waliokuwa raia wa nchi ya Burundi waliopewa uraia wa Nchi ya Tanzania wanaoishi kwenye Makazi hayo kujihusisha na uingizaji wa silaha za kivita, ujambazi na ujagili hali ambayo ilimfanya Rais atowe agizo la kufanyika msako wa mara kwa mara
Social Plugin