Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
RIPOTI kuhusu tuhuma zinazowakabili makatibu wakuu wastaafu wawili(Adbulrahman Kinana na Yusuph Makamba) akiwemo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe tayari imekamilika na inatarajiwa kukabidhiwa kwa Kamati kuu ya Chama cha Mapinduzi mwishoni mwa wiki hii na kamati ndogo ya nidhamu chini ya uongozi wa Makamu Mwenyekiti wa chama, Bara Philip Mangula.
Kauli hiyo ilitolewa jijini hapa jana na Katibu Mkuu wa chama, Dk Bashiru Ally wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala matatu yakiwemo kuanza kwa vikao vya kamati kuu ya chama mwishoni mwa wiki, ziara ya siku tatu mkoani Mtwara na ugeni wa wanachama wapya kujiunga CCM.
Dk. Bashiru alisema kuwa siku saba zilizotolewa na kamati kuu ya chama zimeshamalizika ambapo taarifa hiyo itapitiwa kesho kutwa na kamati ndogo ya nidhamu ya chama ili iwasilishwe kwa kamati kuu mwishoni mwa wiki.
“Kamati kuu itakaa mwishoni mwa wiki hii ili kupokea taarifa ya Mangula hivyo wiki hii wakati vikao vikianza kamati hizo mbili kuu na ndogo ya nidhamu na maadili zitakaa,”alisema Dk. Bashiru.
Alifafanua kuwa uamuzi wa chama ni kuwa taarifa ya Mangula ipo tayari kwa ajili ya kuwasilishwa kwenye vikao vya chama ambapo baada ya vikao Polepole atatangaza kama wamebainika kuwa na makosa na hatua gani zitachukuliwa na kwa adhabu gani.
Alisema yapo makossa mengine ukithibitika adhabu yake haitangazwi na baadala yake anaambiwa mhusika na kwamba saa nyingine inaweza ikatolewa adhabu ya onyo kali hiyo itatangazwa hadharani.Pia unaweza kukosa aina fulani ya haki zako za uanachama .
“Ukithibitika umefanya makosa ya kukiuka kanuni hiyo mtu mwingine anakosa haki za uanachama na kuwa chini ya uangalizi.. lakini wakati mwingine mtu anapewa karipio kuliko onyo kali kama utaratibu wa kulitumikia ana muda wa uangalizi ili ajirekebishe,”
Alifafanua wakati mwingine hupelekea mhusika kuachishwa uanachama na kuwa raia huru lakini anaweza kujiunga tena na kujiunga kwa mujibu wa taratibu za kikanuni na kama ni kiongozi anaweza kusimamishwa uongozi kwa muda au kuachishwa.
Alifafanua kuwa adhabu hizo hutolewa baada ya watuhumiwa kusikilizwa, kujitetetea na baada ya kamati kuu kuchambua na kujiridhisha ili kutoa uamuamuzi.
“Kwa hiyo kuhusu hatua zitakazochukuliwa ni baada ya vikao vya kamati kukaa na kupokea taarifa ndio uamuzi utatolewa, hivyo taarifa ya Mzee Mangula itawasilishwa ndani ya kamati kuu mwisho wa wiki hii,”alisema.
Aidha, Dk. Bashiru amekanusha taarifa zilizosambazwa mtandaoni na baadhi ya watu kuhusu ziara yake mkoani Mtwara kuwa alikuwa akilindwa na askari polisi si za kweli.
“Kuna watu wameshaharibu sifa ya ziara yangu wametengeneza picha inayoonyesha gari la rangi ya kijani wanayoiita ya katibu mkuu halafu imezungukwa na polisi akaandika umoja wa vijana wakimlinda katibu mkuu wa CCM.
"Zipo mamlaka zinazoweza kusimamia matumizi bora ya mtandao nakanusha maana ziara yangu ilifanyika mchana na waandishi wa habari ni mashahidi hivyo tusaidiane kueleza kama ni kweli tulilindwa na viongozi wa dola,”alisema.
Aliongeza: "sio ziara yangu ya kwanza kufanyika mara nyingi huwa Napata ulinzi wa askari wa barabarani ni wa kawaida sina sababu ya kulindwa maana vyombo hivyo vinafanya kazi kwa mujibu wa sheria.
"Wana CCM tutumie vizuri mitandao ya kijamii nimemwelekeza Polepole aeleze sio gari la Katibu Mkuu na ziara ya Mtwara haikuwa hivyo na vyombo husika chukueni hatua."