Benki Kuu ya Tanzania na Benki Kuu ya Zambia zimerasimisha matumizi ya Kwacha ya Zambia na shilingi ya Tanzania kwenye mpaka wa Tunduma na Nakonde ambapo wananchi wataweza kutumia fedha za nchi hizo mbili katika shughuli zao za kila siku za kiuchumi bila kubadilisha.
Akizungumza kwenye hafla hio iliyohudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Nakonde, Mhe. Field Simwinga pamoja na Viongozi wa Serikali na Wakuu wa Taasisi mbalimbali kutoka Zambia na Tanzania, Mkuu wa Wilaya ya Momba, Mhe. Juma Irando alieleza kuwa Urasimishaji wa Matumizi ya Kwacha na Shilingi utaongeza nguvu katika jitihada mbalimbali zilizokwishafanyika ili kuongeza chachu ya biashara katika eneo la mpaka wa Tunduma na Nakonde.
“Utaratibu huu utaondoa mlundikano wa Kwacha upande wa Tanzania. Kama mnavyojua, Wananchi wa Zambia wananunua bidhaa na huduma kwa wingi kutoka Tunduma kwa kutumia Kwacha wakati Watanzania hawawezi kununua vitu kutoka upande wa Zambia (Nakonde) kwa kutumia Shilingi. Kwa sababu hiyo kunakuwa na Kwacha nyingi upande wa Tanzania ambazo hatimaye zinaishia mikononi mwa wauzaji wasio rasmi”
Urasimishaji huo unategemewa kuchochea shughuli za kiuchumi kwa kuwaondolea wananchi gharama za kubadili fedha kwani kuanzia sasa watauza na kununua kwa kutumia Kwacha na Shilingi kwa pamoja.
“Ushiriki wa Benki zetu hapa Mpakani katika kununua na kuuza Kwacha na Shilingi kunawapatia wananchi huduma salama za ubadilishaji wa fedha, ambapo wataepusha hatari ya Wananchi kupewa fedha bandia. Pia benki zitatoa viwango sahihi vya ubadilishanaji wa Kwacha na Shilingi hivyo kulinda thamani ya fedha zetu”, aliongeza.
Mhe. Irando alisema kuwa tukio hilo litaimarisha ushirikiano wa kihistoria kati ya Serikali ya Zambia na Tanzania na kuboresha hali ya maisha ya wananchi kwa kurahisisha shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Uzinduzi wa utaratibu huo ni utekelezaji wa Hati ya Makubaliano (MOU) iliyosainiwa tarehe 21 Septemba 2018, kama jitihada za serikali ya Zambia na Tanzania za kumaliza changamoto ya muda mrefu ya biashara holela ya fedha za kigeni katika mpaka wa Tunduma na Nakonde.