Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MADAKTARI KUKUTANA NA RAIS MAGUFULI KESHO


Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kinatarajia kukutana na kuzungumza na Rais John Magufuli, ambapo miongoni mwa mambo watakayomueleza ni changamoto za ukosefu wa ajira, udhalilishaji na motisha za watumishi.

Rais wa MAT, Dkt. Elisha Osati amesema kuwa mkutano huo unaotarajiwa kufanyika kesho tarehe 20 mwezi huu katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), utashirikisha zaidi ya watumishi 1,000 wa kada ya afya.

“Tunataka tumueleze Rais masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya afya, pamoja na kumpongeza kwa kazi kubwa iliyofanywa na serikali kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini,” amesema Dkt Osati.

Kuhusu tatizo la ajira kwa wahitimu Dkt. Osati amesema kuwa, kila mwaka wahitimu 1,500 wa taaluma ya udaktari wanaingia mtaani na hakuna ajira, lakini taarifa ya wizara ya afya inaeleza kuwa wana upungufu wa madaktari kwa asilimia 51.

Ameshauri kuwa ili kuweza kuondokana na hali hiyo, ni vema serikali ikashirikiana na sekta binafsi katika kujenga vituo vya afya nchini ili kusaidia kutoa ajira na huduma bora na za uhakika kwa wananchi.

Dkt. Osati amesema kwamba kwa viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO), daktari mmoja anapaswa kuhudumia watu 10,000 kwa mwaka, lakini nchini Tanzania daktari mmoja anahudumia watu 25,000 kwa mwaka.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com