Watu wapatao 31 wameuawa hapo jana katika shambulio dhidi ya kijiji cha Ogossagou nchini Mali.
Maafisa wa serikali ya Mali wametangaza habari hiyo baada ya watu wenye silaha kuvamia kijiji hicho katikati ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Maafisa wa eneo hilo wamesema kuwa, watu wenye silaha Alhamisi usiku walikivamia kijiji cha Ogossagou cha katikati ya Mali na kuua watu wasiopungua 31. Wanamgambo wa kabila la Dogon ndio wanaotuhumiwa kufanya mauaji hayo.
Mkuu wa kijiji cha Ogossagou amethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, wanamgambo wapatao 30 walikivamia kijiji hicho baada ya jeshi la serikali kuondoka.
Mwezi Machi mwaka jana pia kijiji hicho kilishuhudia mauaji makubwa ya umati ambayo yalipelekea kuuliwa kwa halaiki watu 160 wa kabila la wafugaji la Fulani.
Licha ya jeshi la Mali kwa kushirikiana na askari wa kigeni kama wa Ufaransa kuchukua hatua mbalimbali, lakini bado nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika inaendelea kushuhudia machafuko na vitendo vya mara kwa mara vya kigaidi.
Social Plugin