Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Philip Mangula ametangaza kuwafyeka mapema wanachama wanaojipitisha kwenye majimbo na kata kabla ya wakati katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu kwa kuwa ni kosa kimaadili.
Mangula ametoa onyo hilo jana katika kongamano la maadhimisho ya miaka 43 ya kuzaliwa CCM jijini Dodoma.
Amesema “Uchaguzi ni mwaka 2020 nafasi bado zina wenye nafasi, Rais bado ni Rais, Mbunge, Diwani bado ni wabunge na madiwani, yeyote anayekwenda kwenye jimbo ambalo bado Mbunge halali hadi kuvunjwa kwa bunge, ukionekana unajipitisha, unanusa nusa huko ni kosa la kimaadili, mwaachie atimize yale aliyotarajiwa kwa kipindi cha miaka mitano.”
Makamu Mwenyekiti huyo, amesema baada ya kuvunjwa bunge ndio jimbo litakuwa wazi na kwamba atayeenda kinyume na hapo atakatwa kabla ya kwenda kwenye mchakato wa kura za maoni.
“Kuna kanuni za uongozi na maadili, zinasema katika kupambana na vitendo vya rushwa wakati wa chaguzi mbalimbali, kiongozi yeyote atakayethibitika ameshinda uchaguzi kutokana na kitendo chochote rushwa atanyang’anywa ushindi atakaopata na pia atazuiwa kugombea nafasi yeyote kugombea tena uchaguzi mwingine wowote kama itakavyoamuriwa na Halmashauri Kuu ya Taifa,”amesema
Mangula amesema katika uchaguzi huo watakuwa makini kupita kiasi.
“Ile ya kwenye jimbo kuchukua fomu watu 10 wanaanza kukimbizana huyu kata ile huyu ile ndio inachochea rushwa na kugawanya watu kwenye makundi, lakini ukute kapata kwa njia haramu kanunua ushindi atanyang’anywa,”
Aliongeza “Mambo yanayozuiwa ni kutoa michango, misaada katika eneo ambalo mwanachama anakusudia kugombea nafasi ya uongozi.Viongozi wa kuchaguliwa wanaruhusiwa kutoa misaada, michango katika kipindi ambacho si cha uchaguzi, mtu mwingine ujitie kimbelembele uende kule tunawachuja kabla hata ya kwenda kuzunguka kwa wananchi.”
Mangula alisema “Tukipata yale majina 10 yanayotaka kuomba jimbo Fulani tunaanza kuangalia, malalamiko ya kujipitisha pitisha toa pembeni huyo, wanakatwa waliobaki sasa tuwajadili hata wakiwa watatu ndivyo tutakavyofanya, walioanza kimbelembele cha kujipitisha.”
Akizungumzia kuhusu amani, Mangula alisema mazingira ya amani yanawekwa serikali na kwamba wachafuzi wa amani ni wanasiasa.
“Badala ya kutizama kanuni na taratibu, kwa mfano kuna watu wamesuasa kutambua serikali za mitaa, wanasema hawakubali, bahati mbaya wanasahau hata historia, nina kumbukumbu mwaka 1994 kulikuwa na vyama vingi CCM ilipata ushindi asilimia 97 ya vitongoji vyote, hakuna aliyegoma, wala mashirika ya kimataifa kusema hakukua na demokrasia,”amesema.
Ameeleza mwaka 1999 CCM ilipata asilimia 88, mwaka 2004 ilipata asilimia 92.4, mwaka 2009 asilimia 91.23, mwaka jana imepata ushindi zaidi ya asilimia 90 lakini zimeibuka kelele kuwa hakuna demokrasia na haki za binadamu.
“Hawa wanafiki hawa, kwanini badala ya kujiuliza kwanini wenzetu wanashinda, nitawapa siri tangu mwanzo tulipopata Uhuru alitoa umuhimu kwa chama baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere baada ya Uhuru alitoka na kwenda kuimarisha chama na kumuita Mzee Kawawa endesha serikali hadi mwaka 1962 ndio akarudi kuwa Rais,”amesema
Amesema CCM ina wanachama zaidi ya milioni 10 ndio nguvu ya chama na pia mfumo na mpangilio ya uongozi inatoa nafasi kwa wanachama kukutana na kutatua matatizo na kushauri na hiyo ndiyo nguzo ya chama.
Social Plugin