Makampuni kumi na tano (15) yaliojumuisha wazalishaji pamoja na wasafirishaji wa bidhaa za Mbogamboga na Matunda wajiongezea fursa katika soko la Ulaya kufuatia Ushiriki wao katika Maonesho ya Kimataifa ya Mbogamboga na Matunda yajulikanayo kama Fruit Logistica 2020 yaliyofanyika tarehe 5 hadi 7 Februari, 2020 mjini Berlin nchini Ujerumani.
Mazao yaliyovutia wanunuzi na wadau wengine katika maonyesho hayo ni pamoja na parachichi, rasiberi, pasheni, ndimu zisizo na mbegu, njegere, snow peas na sugar snaps, maharage machanga (green beans), french Beans, babycarrots, aina mbalimbali za jamii ya pilipili, viungo vya chakula kama vile tangawizi, nana (mint), kitunguu jani (chives), tikiti maji na mafuta ya parachichi.
Taarifa iliyotolewa nchini na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Balozi Dkt. Abdallah S. Possi imeeleza kuwa mafanikio ya ushiriki wa Tanzania yamekuwa mkubwa kutokana na makubaliano ya kimkakati yaliyofikiwa baina ya wafanyabiashara wa Tanzania na wanunuzi wa mbogamboga na matunda wa nchi za Ulaya, hali inayoleta viashiria chanya vya kupata masoko makubwa. Makubaliano hayo yanatarajiwa kuimarisha biashara kati ya Tanzania na nchi za Ulaya, na hivyo kuvutia uwekezaji katika sekta husika nchini.
Wafanyabiashara wameweza kukutana na kuingia makubaliano na wanunuzi, wabia wa biashara na wadau muhimu kama vile Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC) na Taasisi ya Kimataifa ya GLOBALG.A.P inayoshughulikia viwango vya ubora wa bidhaa za kilimo na mifugo. Taasisi hizo ni wadau muhimu katika kuwawezesha wazalishaji kutumia njia salama, sahihi na endelevu katika uzalishaji na kuwaunganisha na masoko ya kikanda na kimataifa. Vilevile washiriki waliweza kujifunza teknolojia za kuzalisha, kusindika, kufungasha, kuhifadhi na kusafirisha mazao ya kilimo ili kukidhi mahitaji ya soko la Ulaya.
“Binafsi nilikutana na mzalishaji kutoka Tanzania ambaye ameingia makubaliano na muwekezaji kutoka Ujerumani. Hii inamaanisha Maonesho haya pia yalikuwa ni fursa kwa wazalishaji wa Tanzania kutafuta wabia wa biashara” amesema Mhe. Balozi Possi.
Aliendelea kusema kuwa, mkakati wa Ubalozi ni kuandaa na kuratibu matukio maalum kama vile Maonesho, Semina, Mikutano ya ana kwa ana ya wafanyabiashara ili kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na wadau muhimu wa nchi za Ulaya. Vilevile, Ubalozi wa Tanzania uliopo Barlin umekuwa ukihimiza ushiriki wa Tanzania katika Maonesho yanayofanyika nchini humo ili kutafuta fursa zaidi za kibiashara.
Mhe. Balozi ameshauri wazalishaji kuimarisha umoja miongoni mwao ili wapate urahisi wa kuwa na wingi wa bidhaa zinazokidhi viwango vya ubora vinavyohitajika katika soko kubwa la Ulaya kwa ujumla wake.
Fruit Logistica ni Maonesho makubwa ya matunda na mbogamboga katika Bara la Ulaya ambayo kwa mwaka huu yamevutia ushiriki wa waoneshaji zaidi ya 3,300 kutoka kila hatua ya mnyororo wa ugavi (supply chain) ambao walitoka katika nchi 93 duniani. Kadhalika, Maonesho yalivutia watembeleaji zaidi ya 78,000 kutoka nchi zaidi ya 135.
Kwa Tanzania, TanTrade kwa kushirikiana na Kituo cha Biashara ya Kimataifa (ITC) na Taasisi inayosimamia Wadau wa Matunda na Mbogamboga, Maua, Viungo vya chakula na Bidhaa zake (TAHA) iliratibu ushiriki wa Tanzania kwenye Maonesho hayo ikiwa ni matokeo ya mafanikio ya utekelezaji wa mradi wa Market Access Upgrade Programme (MARKUP) wenye lengo la kuimarisha upatikanaji wa masoko ili kuongeza mauzo ya nje ya nchi kwa bidhaa za kilimo.