Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MGUMBA: “WAKULIMA WA ZAO LA MUHOGO WALIME KWA TIJA”


Wakulima wa zao la muhogo nchini wameelekezwa kulima kwa tija ili waweze kutosheleza masoko ya ndani na nje ya nchi, huku wakihimizwa kufuata maelekezo ya wataalamu kwenye matumizi sahihi ya mbegu bora na safi badala ya kutumia mbegu yoyote bila kuzingatia hali ya ekolojia.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe Omar Mgumba (Mb) alipokuwa akizindua Umoja wa Wazalishaji na Wasindikaji wa Zao la Muhogo nchini (TACAPPA) katika mkutano wa wadau wa muhogo ulioandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) jijini Dar es Salaam.

Mhe Mgumba amesema kuwa zao la muhogo huzalishwa katika mikoa mbalimbali nchini kutokana na uwezo wake wa kustahimili mazingira tofauti ya ekolojia. Kwa mwaka 2018, muhogo ulikuwa zao la pili kwa uzalishaji yenye asili ya chakula hapa nchini baada ya zao la mahindi na ulichangia zaidi ya asilimia 17 ambapo mahindi ilikuwa asilimia 37 na mchele asilimia 13 katika uzalishaji wa mazao hayo ya chakula.

Aliendelea kueleza kuwa pamoja na uzalishaji huo changamoto kubwa katika zao hilo ni uzalishaji mdogo na wenye tija. Kwa mwaka 2017/2018 uzalishaji wa muhogo ulifikia wastani wa tija ya tani nane kwa hekta moja ambayo iko chini sana ukilinganisha na viwango vya nchi zingine zilipofikia kama Indonesia, Nigeria ambao wao wamefikia zaidi ya tani 21 hadi 30, na hii ndio changamoto kubwa sana inayopelekea kushindwa kushindana katika masoko ya Kimataifa.

“Tija ndogo hutokana na matumizi hafifu ya mbegu bora, kutokuzingatia kanuni za mbegu bora, magonjwa mbalimbali yanayokabili zao hilo hasa batobato na michirizi ya kahawia, ukosefu wa masoko ya uhakika, ubora duni wa bidhaa tunazozalisha ambazo zinashindwa kushindana na bidhaa zingine kwenye soko la Kimataifa, matumizi hafifu ya zana za kilimo katika mnyororo wa thamani na matumizi finyu ya bidhaa za muhogo nchini” amesema Mhe Mgumba.

Ili kutatua changamoto hizo Serikali imeboresha Sheria ya vituo vya utafiti wa mazao mbalimbali, kwa sasa kuna vituo saba maalum ambavyo vinafanya tafiti kwa ajili ya zao la muhogo ili kuja na mbegu bora zenye uwezo wa kupambana na magonjwa,

mabadiliko ya tabia nchi na zenye tija hadi sasa aina ya mbegu 21 zimezinduliwa kwa ajili ya zao la muhogo pekee. Aina tisa za mbegu zilizozinduliwa ni kwa ajili ya ukanda wa kusini, aina nane kwa ajili ya ukanda wa mashariki na aina nne kwa ajili ya ukanda wa Ziwa na magharibi.

Nae Mwakilisha kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, amesema kuwa tarehe 4 Juni, 2018 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli alizundua programu ya kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili iitwayo ASDP II na alielekeza programu hiyo itekelezwe na wadau wote katika mnyororo wa thamani, hivyo muhogo ni kipaumbele kwenye programu hiyo. Hivyo uanzishwaji wa Umoja huu ni utekelezaji wa maelekezo hayo.

Bw Edwin Rutageruka Mkurugenzi, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade. amewasihi wazalishaji wa bidhaa hiyo kujipanga kupitia umoja wao kwa kupenya katika masoko mbalimbali, kuweza kuwahudumia wawekezaji nchini na kuongeza thamani zao hilo.

Ameongeza kwa kusema kuwa TanTrade imesimamia uanzishwaji na usajili wa umoja wa Wazalishaji na Wachakataji wa Muhogo Tanzania baada ya maazimio ya mkutano uliofanyika tarehe 28 Januari, 2019 lengo ni kuwa na sauti ya pamoja katika kuendeleza zao hilo.

Pia Mhe Godwin Gondwe, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Tanga amesema kuwa kwa mkoa wa Tanga wamelichukua kama zao la kimkakati katika kukuza uchumi kupitia kila kaya katika mkoa huo na wameona mafanikio makubwa kupitia zao hilo.

Nae Bi Mwantumu Mahiza Mwenyekiti wa Umoja wa Wazalishaji na Wasindikaji wa Zao la Muhogo nchini (TACAPPA) amesema kwa sasa muhogo ni zao la kilimo cha biashara na sio cha chakula tu, hivyo wakulima waingie kwenye kilimo cha mikataba ili kuondoa udidimizaji kwa wakulima. Pia amehimiza mawakala maarufu kama madalali wajiunge na umoja huo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com