Spika wa bunge la uganda ametoa wito kwa mke wa raia wa Uganda ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Janet Museveni kufika mbele ya chombo hicho cha kutunga sheria kufuatia mkanganyiko kuhusu kuanza kutumika kwa mtaala mpya wa elimu.
Waziri huyo alishindwa kufika mbele ya bunge Jumanne Februari 18 mwaka huu kufuatia wito uliotolewa na Spika Rebecca Kadaga wiki iliyopita.
Licha ya kushindwa kufika alituma udhuru kupitia kwa Waziri wa Elimu ya Msingi, Rosemary Seninde, akiomba kuitikia wito huo Februari 20, 2020.
Hata hivyo spika ametoa wito wa mwisho na kusema kwamba kiongozi huyo ana nafasi moja ya mwisho.
Wabunge nchini Uganda wanaituhumu wizara hiyo kuanza kutumia mtaala mpya kwa wanafunzi wa elimu ya sekondari licha ya bunge kuamuru kusitishwa mpango huo.
Wabunge walizuia mtaala huo kuanza kutumika kutokana na upungufu wa vitabu, na upungufu wa waalimu wenye ujuzi wa kutumia mtaala huo.