Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Tanzania inatakuwa mwenyeji wa Mkutano wa Mawaziri na Wadau wa Utatu wa Sekta ya Ajira na Kazi kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unaotarajiwa kufanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 2 hadi 6 Machi 2020.
Mkutano huu ambao utafunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, umebeba kaulimbiu isemayo “Kukuza Soko la Ajira na Mahusiano Mema Sehemu za Kazi kwa Maendeleo Endelevu”.
Akizungumza na Kamati ya Maandalizi ya Mkutano huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa, Serikali ya Tanzania imejipanga vizuri kuwapokea Mawaziri 15 kutoka Nchi za SADC na kuwataka wajumbe wa Kamati hizo kukamilisha maandalizi kwa kuzingatia viwango ambavyo tayari vimewekwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika mwaka 2019 hapa nchini.
“Tanzania ni Mwenyekiti wa SADC kwa kipindi cha mwaka mmoja. Tumeendelea kuwa na Mikutano kadhaa ya kisekta tangu ulipofanyika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC mwaka 2019. Nawahimiza tuendelee kuandaa mikutano hii kwa kufuata viwango vya juu vilivyowekwa na Mhe. Rais wetu wakati wa Mkutano huo na mingine iliyofuata hadi hapo tutakapokabidhi uenyekiti kwa nchi nyingine” alisisitiza Mhe. Mhagama.
Aidha, Mhe. Mhagama alipokea taarifa za utekelezaji wa majukumu ya kamati ndogo ndogo ikiwa ni pamoja na kupitia ratiba ya Mkutano ambapo mbali na kushiriki Mkutano huo, Mawaziri hao watapata fursa ya kufanya ziara katika maeneo kadhaa ikiwemo Chuo Don Bosco Net Tanzania kilichopo Dar es Salaam kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na vijana wanaosoma chuoni hapo. Pia Mawaziri watatembelea maoneo mbalimbali ya kihistoria yaliyopo Bagamoyo lengo ikiwa ni kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania.
Kadhalika, Mawaziri hao watashuhudia uzinduzi wa Programu ya Taifa ya Mafunzo kwa Vitendo mahala pa kazi kwa vijana (Internship) utakaofanyika tarehe 5 Machi 2020 sambamba na ufunguzi rasmi wa Mkutano huo. Mkutano huu ni mwendelezo wa mikutano ya kisekta ya SADC ambayo itafanyika nchini kwa kipindi cha mwaka mmoja, kufuatia Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo hadi mwezi Agosti 2020.
Mkutano wa Mawaziri ambao utatanguliwa na vikao vya maandalizi vya Makatibu Wakuu na Wataalam vitakavyofanyika kuanzia tarehe 2 Machi 2020, unatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki kutoka nchi 16 wanachama wa SADC ikiwemo Tanzania.