Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira ameagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Zefrin Lubuva asilipwe mshahara wa Februari hadi atakapojirekebisha.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mghwira kukasirishwa na kitendo cha mkurugenzi huyo kushindwa kujibu maswali aliyomuuliza .
"Mkurugenzi naomba kupata taarifa ya makusanyo yenu na kiasi mlichotoa kwa vikundi vya kina mama, vijana na watu wenye ulemavu, mmetoa kwa asilimia ngapi na kwa nini hamjafikia malengo kama Serikali ilivyoelekeza, “alihoji RC Mghwira.
Baada ya swali hilo, mkurugenzi alipewa kipaza sauti ili kujibu lakini alitaka ajibu mtaalamu mwingine jambo ambalo Mghwira alilipinga na kutaka ajibu mwenyewe.
Licha ya kutakiwa kujibu Lubuva alishindwa na kunyamaza kimya na kumfanya mkuu huyo wa Mkoa kumtaka mwenyekiti wa halmashauri hiyo kujibu.
Mwenyekiti wa Halmashauri, Theresia Msuya amesema kutofikia malengo kumetokana na uzembe wa watendaji.
Baada ya maelezo hayo, Mghwira alimtaka tena Lubuva kusimama na kutoa majibu kwa nini hawajafikia lengo la kutoa asilimia 10 kama Serikali inavyoelekeza lakini kwa mara ya pili alishindwa kujibu.
"Mkuu naomba radhi tugange yajayo" alijibu Lubuva na kisha kuketi.
"Sasa wanaokulipa mshahara wasikulipe mwezi huu, tugange yajayo mpaka huo mwezi Machi,” amesema mkuu huyo wa Mkoa.
Sakata hilo limetokea leo Ijumaa Februari 14, katika kikao maalumu cha kamati ya ushauri ya mkoa cha makisio ya mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021, kilichofanyika leo.
Social Plugin