Rais Trump kususia mkono wa Spika Pelosi na Pelosi kumjibu kwa kuichana hotuba yake ni baadhi tu ya vitimbi vilivyodhihirisha mgawanyiko mkali wa kisiasa nchini Marekani, wakati Trump alipotoa hotuba kuhusu hali ya nchi.
Tofauti na ilivyozoeleka kuwa hotuba ya rais wa Marekani kuhusu hali ya nchi ni muda wa maridhiano kisiasa, mazingira katika kikao cha Congress kilichowaleta pamoja wajumbe wa baraza la wawakilishi na maseneta yaliakisi mpasuko mkali wa kisiasa muda wote wa saa moja na dakika 18 wa hotuba ya Trump.
Zoezi zima lilianza vibaya pale Rais Trump alipokataa kuupokea mkono alionyooshewa na spika wa baraza la wawakilishi Bi Nancy Pelosi na kuuacha ukining'inia hewani.
Na lilimalizika kwa hatua ya Pelosi kumjibu Trump mtindo wa jino kwa jino, alipochana vipande vipande nakala ya hotuba ya Trump aliyokuwa amekabidhiwa, mara tu Trump alipomaliza kuzungumza.
Rais Trump ametumia sehemu kubwa ya hotuba yake kwa majigambo, ya namna alivyofanikiwa kuukarabati uchumi wa Marekani, na hadhi ya nchi hiyo, ambavyo amedai vilikuwa vimewekwa rehani na watangulizi wake.
Masuala mengine aliyoyamulika Trump katika hotuba yake, ni makubaliano ya kibiashara kati ya China, na mengine ya eneo huria la kibiashara katika nchi za Amerika Kaskazini, akisema hayo ni mafanikio makubwa ambayo yatarejesha maelefu ya viwanda nchini Marekani.
Amezungumzia pia sera za kupunguza kodi na kumaliza kuhusika kwa majeshi ya Marekani katika mizozo ya Mashariki ya Kati, kama ushahidi wa kutimiza ahadi alizozitoa kwa wapiga kura.
Hotuba yake ilishangiliwa mara kwa mara na wabunge wa chama chake cha Republican waliosimama kumpigia makofi, huku wademocrat wakibakia katika viti vyao, baadhi wakizomea, na wengine hata kutoka nje.
Social Plugin