Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akikagua mifugo 600
iliyolundikana kwenye zizi dogo lenye uwezo wa kuhifadhi ng'ombe 60
alipokwenda kukagua mifugo hiyo iliyokamatwa na Halmashauri ya
Tanganyika Mkoa wa Katavi na kuwatoza faini ya shilingi milioni 60.
Nyuma ni Daktari Mkuu wa Mifugo Tanzania, Profesa Hezron Nonga.
WAZIRI
wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ametoa siku saba kwa Daktari Mkuu wa
Mifugo Tanzania (CVO), Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania (TFS) na Wakili Mkuu wa Serikali wakutane kutathmini na
kuondoa dhuluma zinazoendelea kwa wafugaji pamoja na kuandaa kanuni na
miongozo itakayoweka uwazi katika usimamizi wa Sheria za Misitu na
Mifugo.
Mpina ametoa
agizo hilo mwishoni mwa wiki baada ya Halmashauri ya Wilaya ya
Tanganyika Mkoa wa Katavi kutoza faini ya shilingi milioni 60 sawa na
shilingi laki moja kwa kila ng’ombe baada ya ng’ombe 600 kukamatwa
wakichungwa ndani ya Msitu wa Tongwe Mashariki unaomilikiwa na
halmashauri hiyo.
Waziri
Mpina amefikia hatua hiyo baada ya kuwepo ukiukwaji mkubwa wa sheria na
ukamataji holela wa mifugo unaofanywa kwenye baadhi ya Halmashauri,
Hifadhi za Wanyama, Mapori ya Akiba ambapo mifugo inapokamatwa hunyimwa
huduma muhimu ikiwemo malisho, maji, chanjo na dawa hali inayosababisha
mifugo mingi kudhoofika na kufa.
Alibainisha
manyanyaso mengine ni wafugaji kutozwa faini kubwa ambazo hazipo kwa
mujibu wa sheria, kupigwa, mifugo kuibiwa, kupigwa risasi na mingine
kuuzwa kwa njia ya mnada kwa kisingizio cha kukosekana mmiliki wa
mifugo hiyo huku idadi inayotajwa mahakamani ni ndogo ikilinganishwa na
mifugo iliyokamatwa.
Akizungumza
mara baada ya kufika eneo ilikoshikiliwa mifugo hiyo umbali wa zaidi ya
kilomita 50 kutoka barabara ya Mpanda- Kigoma, Waziri Mpina alihoji
iweje Halmashauri hiyo iache kufuata sheria za nchi zinavyoelekeza kwa
watu wanaoingiza mifugo na badala yake wakabuni faini ya kutoka kichwani
kinyume cha Sheria na kuitafsiri hatua hiyo kuwa ni Unonevu, Rushwa,
Wizi, Dhuluma na Manyanyaso kwa wafugaji.
Waziri
Mpina alisema yeye kama msimamizi mkuu wa Sekta ya Mifugo nchini hawezi
kumtetea mfugaji anayevunja sheria kwa kuingiza mifugo kwenye maeneo
yaliyokatazwa kisheria lakini kilichomfanya kuingilia kati suala hilo ni
kuvunjwa kwa Sheria ya Misitu Namba 14 ya mwaka 2002 inayoeleza bayana
kwamba mtu atakayekutwa ametenda kosa ndani ya msitu atatozwa faini ya
shilingi 30,000 na isiyozidi milioni moja.
“Kutoza
hela ambayo haiko kwenye Sheria ni Wizi, ni Manyanyaso kwa wafugaji,
Rushwa huwezi kutoza hela ya Serikali ambayo haiko kwenye kanuni yaani
Serikali iache kusimamia sheria ifanyie kazi maamuzi ya vikao” alihoji
Waziri Mpina.
Mmoja wa
wachungaji hao Koye Mmela alilamikia kitendo cha kukamatwa na
kushikiliwa msituni kwa siku sita mfululizo bila kufikishwa Mahakamani
jambo walilolitaja ni uonevu mkubwa waliofanyiwa na askari waliokuwa
doria.
Mwanasheria wa
Halmashauri ya Tanganyika, Maraka Mrisho alimweza Waziri Mpina kuwa
faini hiyo ya milioni 60 haipo kwenye sheria yoyote bali ilitozwa
kufuatia makubaliano ya kikao kilichowahusisha Maofisa wa Misitu wa
halmashauri pamoja na Maofisa wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) wa
kanda hiyo na kubariki faini ya shilingi laki moja kwa kila ng’ombe.
Mrisho
alisema kwa mujibu wa Sheria ya Misitu Namba Sheria ya Misitu Namba 14
ya Mwaka 2002, kifungu cha 84 Kifungu kidogo cha tano kinasema mtu
yeyote atakayekutwa na kosa ndani ya misitu atatakiwa kulipa faini
isiyopungua shilingi 30,000 na isiyozidi sh. Milioni 1 hivyo hakuna
kifungu kinachozungumia kutoza faini ng’ombe.
Kwa
upande wake Daktari Mkuu wa Mifugo Tanzania (CVO), Profesa Hezron
Nonga amesema waliokamata mifugo hiyo wamevunja Sheria ya Magonjwa ya
Wanyama Namba 17 ya mwaka 2003, Sheria ya Ustawi wa Wanyama Namba 19 ya
mwaka 2008 kutokana na ng’ombe 600 kulundikana kwenye zizi dogo
linalotosha ng’ombe 60 tu hali iliyosababisha mifugo kukosa hewa na
kufa, ndama kukanyagwa, kujeruhiwa na kufa.
Prof.
Nonga alisema ng’ombe hao wamefungiwa zizini muda mrefu bila maji wala
malisho hali iliyopelekea afya zao kudhoofika, utaratibu wa ukamataji
mifugo haukufuatwa kwa kuwa haukuhusisha daktari wa mifugo kama sheria
inavyoelekeza huku mifugo hiyo ikinyimwa chanjo na tiba hivyo
waliohusika na ukamataji huo walitakiwa kukamatwa na kushtakiwa kwa
mujibu wa sheria hizo.
Naye
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Rojaz Romuli alisema
halmashauri hiyo haina bajeti ya kutibu mifugo pindi inapokamatwa
msituni bali jukumu lao ni kulinda misitu isiharibiwe na wavamizi
wakiwemo wafugaji na wawindaji haramu.
Hivyo
baada ya mazungumzo ya kina ya kisheria na kubainika kulikuwa na
ukiukwaji mkubwa wa sheria ndipo Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Tanganyika, Rojazi Romuli akalazimika kubatilisha adhabu hiyo na
kuwatoza faini ya shilingi milioni 11 badala ya shilingi milioni 60 ya
hapo awali.
Kwa muda
mrefu wafugaji wa Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi wamekuwa
wakilalamikia kunyanyaswa, kuteswa kupigwa faini kubwa na hata kuuwawa
na kwamba malalamiko hayo yalishatolewa Rais Dk. John Magufuli
alipofanya ziara mkoani Katavi mwaka jana.
Pia
malalamiko ya aina hiyo yalitolewa kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Luhaga Mpina na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera waliposhiriki
uzinduzi uogeshaji mifugo Halmashauri ya Mpwimbwe mkoani Katavi.
Homera
alilazimika kuchukua hotuba nzima iliyojaa ya malalamiko ya wafugaji na
kuikabidhi kwa Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) Mkoa wa Katavi kwa hatua zaidi lakini bado Halmashauri ya
Tanganyika imeendeleza manyanyaso kwa wafugaji kwa kuwatoza faini kubwa
ambazo haziko kwa mujibu wa sheria.