Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NCHI ZA SADC ZATAKIWA KUTATHMINI UCHUMI WAKE BILA KUTEGEMEA MASHIRIKA YA KIMATAIFA PEKEE

Na Peter Haule na Josephine Majura, WFM, Dodoma

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amesema kuwa nchi za Afrika hasa zilizopo chini ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) zinatakiwa kujitazama na kushauriana kuhusu mwenendo wao wa uchumi badala ya kuyaachia Mashirika ya Kimataifa pekee.

Rai hiyo imetolewa Jijini Dodoma wakati wa Mkutano kati yake na Ujumbe wa SADC unaoongozwa na Bw. Sikumbuzo Dlamini, ambao umetembelea nchini kwa ajili ya Mpango wa kujitathmini kiuchumi kwa mwaka wa Fedha 2019/20.

Dkt. Mpango alisema kuwa nchi za Afrika zimezoea kuona Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) au kuja kuangalia namna gani Uchumi unavyoendelea ili hali   Afrika hasa nchi za SADC zina fursa pia ya kutembeleana na kushaurina namna bora ya kuendeleza uchumi na kuwahudumia wananchi ikizingatiwa kuwa nchi hizo zinafahamiana vizuri.

“Madhumuni ya ujumbe wa SADC kutembelea nchini ni kuangalia hali ya ukuaji wa uchumi, ubadilishanaji wa fedha za kigeni, mauzo ya bidhaa ndani na nje ya nchi na kushauri mahali ambapo Tanzania haijafanya vizuri au kutumia fursa ipasavyo’’, alieleza Dkt. Mpango.

Alisema kuwa nchi za SADC zilikubaliana kuchagua ujumbe ambao utakuja nchini kufuatilia namna uchumi Mkuu unavyoendelea, hivyo ametumia fursa hiyo kueleza utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya Umeme wa Maporomoko ya Mto Rufiji, ujenzi wa Reli kwa kiwango cha Kimataifa (SGR) na miundombinu mingine ya barabara.

Kwa upande wake Kiongozi wa Ujumbe wa SADC, Bw. Sikumbuzo Dlamini, ambaye pia ni Meneja wa Sera za Uchumi na Takwimu wa Benki Kuu ya Eswatini, ameipongez Tanzania kwa maendeleo makubwa iliyofikia baada ya kujionea miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya Reli, miradi ya maji ambayo itasaidia ukuaji wa uchumi Uchumi Mkubwa na kuiwezesha kufikia Malengo ya Maendeleo endelevu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com