Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BINTI ALIYEVUNJA NDOA YA WAZAZI ASOME ASIMULIA ALIVYOFANIKIWA KUWA KIONGOZI MWANAMKE KIJIJINI


Anjelina Mahona 

Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Ni nadra sana kwa maeneo ya vijijini mkoani Shinyanga kuona mwanamke anapewa nafasi ya kuwa kiongozi,na wakati mwingine mwanamke anayefanikiwa kuwa kiongozi huonekana ni mtu wa ajabu na kutokana na mila na desturi kandamizi baadhi ya watu humchukulia mwanamke huyo kuwa ni Malaya hafai kuwa kiongozi!

Malunde 1 blog imekutana na Anjelina Mahona (31) ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nhobola kijiji  cha Bulimba kata ya Ukenyenge wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga anaeleza namna alivyofanikiwa kuwa kiongozi na changamoto mbalimbali alizokutana nazo tangu alipoanza kuwania uongozi mwaka 2011 akiwa ni binti mwenye umri wa miaka 22 tu.

JE ANGELINA MAHONA NI NANI?
Anjelina Mahona amezaliwa kijiji cha Bulimba kata ya Ukenyenge wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga mwaka 1989. ameolewa,ni mama wa watoto wanne na ni mtoto wa tano katika familia ya watoto 9.

Anjelina alihitimu elimu ya darasa la saba mwaka 2004 katika shule ya msingi Bulimba lakini pamoja na uwezo  wake mzuri darasani hakufanikiwa kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza kutokana baba mzazi wake kukataa kumsomesha.

Mwaka 2011 alichaguliwa kuwa Mjumbe wa serikali ya kijiji cha Bulimba hadi mwaka 2019 akiwa ni Mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mwaka 2019 Tanzania ilifanya uchaguzi wa viongozi wa serikai za mitaa ambapo Anjelina aligombea  nafasi ya Mwenyekiti wa kitongoji cha Nhobola kilichopo katika kijiji cha Bulimba na kufanikiwa kuwabwaga wanaume wanne aliokuwa anachuana nao ndani ya chama na akafanikiwa kushinda katika uchaguzi.

Mbali na kuwa mwenyekiti wa Kitongoji cha Nhobola Anjelina anamiliki Kanisa,ni Mwinjilisti  Kiongozi katika kanisa la KKKT Bulimba,alilolianzisha yeye mwenyewe na sasa kanisa lina waumini zaidi ya 80.

MAISHA YA ANJELINA KUELEKEA KWENYE UONGOZI
Anjelina anasema yeye ni miongoni mwa wanawake ambao kamwe hawawez kusahau athari za mfumo dume,mila na desturi kandamizi zinamfanya mtoto wa kike abaguliwe,aonekane kuwa ni mtu wa kuolewa tu hatakiwi kwenda shule.

“Nilihitimu elimu ya darasa la saba mwaka 2004 katika shule ya msingi Bulimba, Nikiwa shuleni nilikuwa na ufaulu mzuri nilikuwa nashika nafasi ya kwanza kuanzia darasa la kwanza hadi la  saba lakini kutokana na mfumo dume baba na mama hasa baba hakutaka nisome.

Siku moja  mwaka 2005 mama alinichukua na kunipeleka kwa mjomba katika kata ya Maganzo wilayani Kishapu lakini asubuhi yake baba alinifuata na kunirudisha nyumbani,baada ya kufika nyumbani ulitokea ugomvi mkubwa hadi ndoa ya baba na mama ikavunjika kwa sababu yangu,mama alitaka nisome,baba alitaka niolewe tu”,anasimulia.

Anjelina anasema mgogoro huo wa wazazi wake hatausahau kwani bado anaamini kuwa yeye ndiyo sababu ya ndoa ya wazazi wake kuvunjika.

“Kutokana na changamoto hiyo,ilinilazimu tu kukaa nyumbani nikajikuta nimeanzisha mahusiano ya kimapenzi na kijana mmoja na mwisho wa siku nikapata ujauzito. Yule kijana akakubali kunioa nikaanza kuishi naye nyumbani kwao/ukweni mwaka 2007.

“Mama mkwe alikuwa mkristo,nikiwa ukweni nikawa nasali baadaye nikaenda kusoma Chuo  cha Biblia cha ‘Bishop Makala’ kilichopo Negezi Kishapu,nikaanzisha Jumuiya katika Kitongoji  cha Bulimba na sasa nina kanisa”,anasimulia Anjelina.

Anjelina anasema kutokana na kuwa na dhamira ya kuwa kiongozi na kujiamini kwake kuwa anaweza kuwa kiongozi mwanamke,Mwaka 2011 alichaguliwa kuwa mjumbe wa serikali ya kijiji cha Bulimba.

Nguvu ya kujiamini na kujitambua zaidi kwa Anjelina iliongezeka maradufu mwaka 2015  baada ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kufika wilayani Kishapu na kutoa elimu ya uraghbishi na mafunzo  mbalimbali kuhusu haki ya mwanamke.

“Kupitia ujuzi na elimu tuliyopatiwa kuhusu haki za wanawake,nilifanikiwa kujisimamia na kuwashauri wanawake wenzangu njia za kuondokana na maisha tegemezi na kumtoa mtu katika hali ya chini na kukabiliana na mila na desturi zinazomkandamiza mwanamke”,anasema Anjelina.

Kutokana dhamira na nia aliyokuwa nayo ya kuwa kiongozi,Anjelina alijitosa kugombea nafasi ya mwenyekiti wa Kitongoji cha Nhobola na kufanikiwa kunyakua nafasi hiyo mwaka 2019 nafasi ambayo anaendelea nayo mpaka sasa.

SABABU ZA MAFANIKIO YAKE NI ZIPI?
Anjelina anasema amefanikiwa kuwa kiongozi kutokana na kuwa na kiu ya kutetea wanawake wanaokandamizwa na mila na desturi kandamizi ambapo yeye ni muathirika wa mila hizo zinazomfanya mwanamke kutopewa haki ya elimu na hata nafasi za uongozi.

“Dhamira na nia ya kuwa kiongozi wa mfano ndiyo vimenifanya niwe na ujasiri wa kusimama mbele za watu na kuzungumza,nimekuwa mstari wa mbele kukemea mila na desturi zinazokandamiza mwanamke.Mimi ni muathirika wa mila hizo.Nilisababisha ndoa ya wazazi wangu ivunjike,baba hakutaka nisome,yeye alitaka niolewe”,anaeleza Anjelina.

“Niliomba uongozi nikiwa na dhamira ya uongozi nikiwa binti wa miaka 22. Nilikuwa mdogo lakini nilipata ujasiri wa kujieleza,nashukuru nimeolewa na mwanaume mwenye busara ananipa ushirikiano lakini pia jamii imekuwa bega kwa bega nami kwa sababu ninafanya kazi zinazowaletea maendeleo wananchi hivyo wananiamini kuwa kiongozi wao”,ameongeza Anjelina.

CHANGAMOTO ALIZOPITIA
Pamoja na kufanikiwa kuwa kiongozi wa serikali ya kijiji na kitongoji, Kauli za kubezwa kuwa mwanamke hawezi kuwa kiongozi,mwanamke akiwa kiongozi atakuwa Malaya na nyinginezo,Anjelina anasema zimekuwa chukizo kubwa kwake.

“Mimi nilianza kuwa kiongozi nikiwa na umri wa miaka 22,nikiwa mjumbe wa serikali ya kijiji.Changamoto kuwa ni kubezwa kuwa mwanamke hawezi kuwa kiongozi.Kuna baadhi ya watu wakikuona umebadilisha mavazi wanasema wewe ni Malaya hali ambayo kama hauna dhamira ya kweli kuwa kiongozi lazima ukate tamaa kwani unafanywa uonekane hufai”,amesema.

Anjelina anaeleza kuwa changamoto ambayo hataisahau ile ya baadhi ya ndugu zake kumpiga vita kuwa hawezi kuwa kiongozi,kwanza yeye ni mwanamke lakini yeye ni binti mdogo hawezi kuwa kiongozi.

“Mfano katika uchaguzi wa mwenyekiti wa kitongoji cha Nhobola mwaka 2019, kati ya wagombea watano ndani ya CCM  wanne walikuwa wanaume,mmoja  kati yao alikuwa baba yangu mkubwa,aliposhindwa akaanza kuniponda akisema ‘Huyu ni binti mdogo atawamalizia jela kwa sababu anajiamini sana…hata hivyo nilimfuata nikwambia anachofanya siyo kitu kizuri”,anasimulia Anjelina.

WITO WA ANJELINA KWA WANAWAKE NA JAMII
Anjelina anatoa wito kwa wanawake wenye nia ya kuwa viongozi kujiamini na kutokata tama huku akibainisha kuwa kinachokwamisha wanawake ni kutojiamini na uwepo wa mila na desturi kandamizi.

“Wanawake wanatakiwa wajisimamie,wajitambue kuwa wao ni viongozi kuanzia ngazi ya familia hivyo wanawake kuwa viongozi. Ukiwa na dhamira ya uongozi, imani na ukajiamini utashinda.Jitahidi kushirikisha mme wako,familia yako na watu wanaokuzunguka ili wakupe ushauri”,anashauri Anjelina.

Katika hatua nyingine Anjelina anasema kupitia uenyekiti wake wanawake wengi wameanza kujitokeza kugombea nafasi za uongozi mfano katika kijiji cha Bulimba kabla ya mwaka 2011 hadi 2015 wanawake viongozi walikuwa wawili tu lakini sasa wapo wanne.

“Nashukuru wanawake tunazidi kujitokeza kugombea na kushika nafasi za uongozi na jamii inaendelea kutumiani na kutuunga mkono. Leo hii kwa jinsi jamii inavyouamini uongozi wangu hata nikitaka kugombea udiwani naweza maana sifa za uongozi ninazo.Mimi nimeanzia chini nitaendelea kupanda”,anasema.

Aidha ameshauri wazee wasing’ang’anie vyeo wawaachie vijana wawe viongozi ili kuongeza kasi ya maendeleo katika jamii huku akiwaomba wanaume kuwaunga mkono wanawake  wenye sifa za kuwa viongozi kwani uongozi siyo misuli bali ni akili,busara na hekima.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com