Kundi la nzige wa jangwani limeingia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ikiwa ni mara ya kwanza kwa wadudu hao hatari kuonekana katika taifa la Afrika ya Kati tangu mwaka 1944.
Shirika hilo la chakula FAO aidha limeonya juu ya kitisho kikubwa cha njaa katika mataifa ya Afrika Mashariki baada ya kuvamiwa na nzige hao.
Kenya, Somalia na Uganda zimekuwa zikipambana na wadudu hao, katika mripuko mbaya kabisa wa nzige ambao maeneo kadhaa ya ukanda huo yalishuhudia miaka 70 iliyopita.
Umoja wa Mataifa umesema nzige hao wa jangwani pia wameonekana Djibout, Eritrea na katika siku za karibuni wamefika Sudan Kusini, taifa ambalo kwa takribani nusu ya idadi ya watu wake tayari wanakabiliwa na njaa baada ya miaka kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa jana jioni na mkurugenzi mkuu wa FAO Qu Dongyu, mkuu wa shirika la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa Mark Lowcock na mkurugenzi mtendaji wa mpango wa chakula duniani, WFP, David Beasley, imefananisha kundi hilo la nzige kama janga la kiwango kilichozungumziwa katika bibilia na linalokumbushia hatari inayoukabili ukanda huo.
Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Stephane Dujarric, akiwa mjini New York hapo jana amezungumza mwito wa ufadhili uliotolewa na FAO wa dola milioni 76 wa kupambana na wadudu hao, ambao hata hivyo unatekelezwa kwa kasi ndogo.
"Maafisa wameomba msaada huo wakati nzige walipoendelea kuvamia kote mashariki mwa Afrika. Gharama za kukabiliana nao zimeongezeka mara mbili hadi dola milioni 138. Mpango wa chakula umeonya gharama za kupambana na athari za nzige kwenye usalama wa chakula tu, zinaweza kuwa mara 15 zaidi ya gharama ya kuwazuia kusambaa. Hadi sasa ni dola milioni 33 tu zimetolewa au kuahidiwa."amesema Dujarric.
FAO imesema nzige waliozeeka , wanaoletwa kwa sehemu na upepo, waliwasili katika pwani magharibi mwa ziwa Albert, karibu na mji wa Bunia mashariki mwa Congo siku ya Ijumaa. Taifa hilo halijawahi kushuhudia nzige kwa miaka 75.