RC SONGWE AAGIZA POLISI ALIYEKAMATWA NA MAGENDO ACHUKULIWE HATUA HARAKA


Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ameagiza Afisa wa Jeshi la Polisi wa Tunduma aliyekamatwa na gari alilomiliki kwa njia za magendo, achukuliwe hatua za kisheria haraka.

Brig. Jen. Mwangela ametoa agizo hilo mara baada ya kukagua magari na bidhaa zilizokamatwa na Mamlaka ya Mapato katika Mpaka wa Tunduma ambapo pia ameonyeshwa gari la Afisa wa Jeshi la Polisi wa Tunduma lililo kamatwa kwa kulimiliki kwa njia za magendo huku taarifa zikionyesha linasafirishwa kuelekea Nchi jirani ya Kongo.

“Afisa huyo wa Polisi amesema kuwa gari hilo lilikuwa likitumika na Jeshi la Polisi kwa kazi maalum lakini nimezungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa amesema gari hilo haliko katika utaratibu wa kipolisi wala halikuwa likifanya kazi za serikali hivyo naagiza achukuliwe hatua za kisheria haraka sana.”, amesema Brig. Jen. Mwangela.

Amesema kwa kumiliki gari hilo kinyume na sheria na taratibu za Nchi kisha kudanganya uhalali wa umiliki wake Afisa huyo wa Polisi anavunja sheria za Nchi, anakwepa kodi, ana hujumu uchumi wa taifa na pia amelitia aibu Jeshi la Polisi.

Brig. Jen. Mwangela  ameongeza kwa kuitaka Mamlaka ya Mapato Mkoa wa Songwe kuhakikisha wana wakamata wote wanaokiuka sheria za Nchi hata kama ni watumishi wa serikali huku akiviagiza vyombo vya ulinzi na usalama Mkoa wa Songwe kuongeza ulinzi katika eneo la Mpaka ili kuzuia Magendo.

Pia amewakumbusha wananchi na wafanyabiashara wanaovusha bidhaa nchi Jirani wafuate taratibu za Forodha, wananchi nao watoe taarifa za wale wanao kiuka sheria kwakuwa watakao kamatwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Naye Kaimu Meneja Msaidizi wa Forodha Mkoa wa Songwe Anangisye Mtafya amesema wamekuwa wakikamata magari ya magendo na mengine ambayo Watanzania wasio waaminifu wamekuwa wakiyabadilisha na kuweka namba zisizo halisi.

Mtafya ameongeza kuwa baada ya kusafishwa Mpaka wa Tanzania na Zambia eneo la Tunduma kazi ya kukamata watorosha magendo imerahisishwa tofauti na zamani ambapo nyumba zilikuwa zimejaa eneo la mpaka.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amefanya ukaguzi wa kushtukiza katika maduka ya biashara jirani na Mpaka wa Tanzania na Zambia eneo la Tunduma na kukuta baadhi ya wafanyabiashara wakiuza mbolea ya Ruzuku nchi jirani ya Zambia huku wengine wakitoa risiti zenye udanganyifu.

Brig. Jen. Mwangela ameagiza kufungwa kwa duka la pembejeo ambalo alimkuta mfanyabiashara Issa Sanga akijaribu kuvusha mbolea ya Ruzuku Nchi jirani ya Zambia na uchunguzi ufanyike ni mbolea kiasi gani amevusha hadi sasa.

 



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post