Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS MAGUFULI AKERWA NA WAPELELEZI KUCHELEWESHA KESI ZA WATU


Rais John Magufuli amesema wapelelezi wa kesi na wasimamizi wa sheria nchini wanawaumiza mahabusi wengi kutokana na kuchelewa kukamilisha kazi kwa wakati.


Amesema wapelelezi wa kesi ni chanzo cha watu kuwekwa kwenye magereza bila hatia yoyote, huku wengine wakiwekwa mahabusi kutokana na shinikizo la matajiri.

Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria iliyokuwa na kaulimbiu, Uwekezaji na biashara: Wajibu wa Mahakama na wadau kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji.

Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli aliwataka viongozi wa dini nchini kuwaombea wapelelezi wanaofanya vitendo hivyo wapate laana.

Alisema idadi ya wafungwa waliopo katika magereza nchini ni ndogo kulinganisha na mahabusi waliopo, ambayo alitaja wafungwa ni 13,455 wakati mahabusi ni 17,632.

Alisema idadi ya mahabusi walioachiwa na Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) baada ya kubainika kubambikiziwa kesi ni 1,422.

“Lakini niwaombe ndugu zangu wapelelezi, ufalme wa mbinguni utakuwa shida kwenu msipotubu kwa Mungu, kwa sababu roho za wasiokuwa na hatia zinaangamia kule, mnawapa shida sana mahakimu na majaji na roho za watu, ninawaambia ukweli mtaenda kuyalipa badilikeni,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:

“Mimi nimeshuhudia ukienda kwenye magereza yetu watu wanalia na wengine ni kesi za kusingiziwa, wapo wengine wamewekwa kule ndani kwa sababu ya matajiri kwamba ni akukomeshe utaenda kwanza mahabusu,” alisema Rais Magufuli.

“Roho za watu wasiokuwa na hatia zinaangamia kule gerezani na wala msiwasingizie majaji na mahakimu kwa sababu hamuwapelekei na saa nyingine hata kupelekwa mahakani ni lazima uhonge ili kesi yako isomwe, mnawapa shida mahakimu na majaji ninawaambia ukweli mtakwenda kuyalipa badilikeni.”

Rais Magufuli alisema idadi ya wafungwa waliosamehewa katika kipindi cha miaka minne ni 38,801 na baadhi yao walikuwa na kifungo cha maisha.

Alisema kwa sasa serikali iko katika mazungumzo ya kuwarejesha wafungwa raia wa kigeni wakiwamo kutoka Ethiopia 1,451 ili warudi kwao.

“Tunafanya mazungumzo na ninafikiri nitasaini hati mapema ndani ya siku mbili tatu ili hawa wafungwa waweze kurudishwa kwao na hii pia itatusaidia kupunguza wafungwa wanaokaa mahakamani,” alisema Rais Magufuli.

Kadhalika, alisema miongoni mwa kero ambazo alizipokea kipindi cha kampeni mwaka 2015 ni pamoja na wananchi wengi kulalamika ucheleweshaji wa kesi, kukithiri kwa vitendo vya rushwa, ubambikizaji wa kesi, ucheleweshaji wa upelelezi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com