Rais wa Tanzania, John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Msomi na Mwanajumuia wa Afrika (Pan-Africanist) Profesa Patrick Lumumba, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli na Profesa Lumumba ambaye ni raia wa Kenya wamezungumzia masuala mbalimbali yahusuyo juhudi za Afrika katika kuimarisha uchumi kwa kutumia rasilimali zake .
Pia wajibu wa Waafrika na viongozi wao katika kuimarisha huduma za kijamii na kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Rais Magufuli amempongeza Profesa Lumumba kwa juhudi zake za kueleza waziwazi makosa yanayosababisha nchi za Afrika kubaki nyuma kiuchumi, kijamii na kisiasa, wajibu wa viongozi na wananchi wa Afrika katika kukabiliana na changamoto zinazozikabili nchi zao na mapenzi yake makubwa kwa Afrika.
Rais Magufuli amemueleza juhudi ambazo Serikali inazifanya katika kujenga uchumi imara wa kujitegemea ikiwamo utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama vile ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa Bwawa la Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 za umeme na kuongeza usambazaji wa umeme kutoka vijiji 2,018 hadi kufikia vijiji 8,587.
Pia, ujenzi wa barabara na madaraja makubwa na madogo, kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari, kuongeza mikopo ya elimu ya juu, kuongeza ukusanyaji wa mapato, kudhibiti rasilimali muhimu ya madini na kupambana na rushwa.
“Mimi sijawahi kukutana nawe kabla, lakini nakusikia na kukuona kupitia vyombo vya habari jinsi unavyopaza sauti kuhusu Bara la Afrika, nakupongeza kwa juhudi hizo, na ninafarijika kwamba unaisemea vizuri Afrika,” amesema Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Profesa Lumumba amemshukuru Rais Magufuli kwa kutenga muda wake kuzungumza naye na amempongeza kwa juhudi kubwa alizozionesha katika kipindi kifupi cha uongozi wake wa miaka minne ambapo ameonyesha mfano wa namna ya kupigania rasilimali za nchi ikiwemo madini, kujenga nidhamu ya utumishi Serikalini, kuimarisha uchumi, kupambana na wizi wa mali za umma, rushwa na ufisadi.
Profesa Lumumba amesema inafaa kwa nchi za Afrika kujifunza mambo yanayofanyika Tanzania kwa sasa na amesisitiza kuwa ni muhimu kwa Waafrika kujiamini na kuchukua hatua madhubuti za kuwaondoa katika hali ya sasa ambapo rasilimali zake zinachukuliwa na Mataifa ya nje ilihali wananchi wake wakikabiliwa na changamoto mbalimbali.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na Mwakilishi wa Kansela wa Ujerumani anayeshughulikia masuala ya Afrika, Guenter Nooke, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Nooke amewasilisha ujumbe wa Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel na pia ameelezea kufurahishwa kwake na hatua kubwa za maendeleo zilizofikiwa hapa nchini ikilinganishwa na alipokuja miaka iliyopita.
Pia amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali katika kupambana na rushwa na kuimarisha uchumi ambapo ameahidi kuwa Ujerumani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji na biashara na masuala mengine ya kijamii.
Kwa upande wake, Rais Magufuli amemhakikishia Kansela wa Ujerumani kuwa Serikali ipo tayari kuuendeleza na kuukuza zaidi uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati yake na Ujerumani, na inawakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kuja kuwekeza hapa nchini.
Katika mazungumzo hayo, Nooke ameongoza na Balozi wa Ujerumani hapa nchini Regine Hess.