Na WAMJW – Dar Es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli ametoa kibali kwa Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inayoongozwa na Mhe. Kapteni Mstaafu George Mkuchika kuajiri madaktari 1000.
Rais Magufuli ametoa kibali hicho jana alpohudhuria maadhimisho ya siku ya madaktari katika ukumbi wa mikutanao wa kimataifa wa Julius Nyerere.
“Ninafahamu kuna madaktari 2700 bado hawajaajiriwa, nitalifanyia kazi” alisema Rais Magufuli na kuendelea kwa kumuuliza Waziri Mkuchika uwezekano wa kuajiri Madaktari 1000.
“Tuajiri madaktari 1000 na wasambazwe vizuri katika Mikoa yote” alisema Rasi Magufuli kauli ambayo ilipokelewa kwa furaha na shangwe kutoka kwa wajumbe waliohudhuria Mkutano huo wa 55 wa Chama cha madaktari Tanzania (MAT)
Rais Magufuli amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imewekeza nguvu kubwa kwenye Sekta ya Afya nchini kwa kujenga miundombinu (majengo) pamoja na ununuzi wa vifaatiba na mashine za kitaalam na kusema kuwa bila ya kuwa na wataalam wa kutosha bado Sekta ya Afya itakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa huduma bora za afya.
“Tuanze na madaktari 1000, mambo yakiwa vizuri tena tutaajiri wengine, tunahitaji madaktari mpaka vijijni, tumejenga vituo vya afya 352 tumejenga Hospitali za Wilaya 77 zote hizi zinahitaji madaktari” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli ameonyeshwa kufurahishwa na utendaji kazi wa madaktari ambao wanatumia muda mwingi kuokoa maisha ya watanzania na kuwaahidi kuzishughulikia changamoto walizonazo ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.