Rais Magufuli amewaonya viongozi wa kisiasa kuacha vitendo vya kuwaweka ndani madaktari hata kwa makosa madogo, vitendo ambavyo amesema yeye hakubaliani navyo.
Rais ametoa kauli hiyo jana alipokuwa akihutubia mamia ya madaktari waliokusanyika katika ukumbi kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) ikiwa ni maadhmisho ya Siku ya Madaktari Tanzania mwaka 2020.
“Nasisitiza Viongozi msipende kuwekaweka Watu ndani, hawa Madaktari mkiwaweka ndani na wao mkiwakuta Hospitali watawaweka ndani pia, anauliza tu nani huyo anaumwa wakisema ni DC au RC fulani anasema muache hapo kwanza, ila na nyinyi Madaktari msije mkafanya hivyo ni dhambi”” alisema Rais Magufuli.
Hata hivyo Rais amesema kuwa onyo hilo alilolitoa sio kigezo cha kwamba madaktari hawatowekwa ndani endapo watatenda makosa, huku akitolea mfano wa daktari anayedaiwa kumbaka mjamzito na kusema kwamba, daktari anayefanya vitendo kama hivyo, hata akiwekwa ndani, madaktari wenzake wasilalamike.
Kuhusu wataalamu kutoka sekta nyingine alisema, “Na hii sio kwa madaktari tu, hata kwa wahandisi na walimu, haiwezekani kila mtu wewe unaweka ndani”
Aidha, Rais amekiagiza Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kuwaonya na kuwachukulia hatua madaktari wachache wanaoshindwa kutumia taaluma zao vizuri, kabla hawajashughulikiwa na wanasiasa.
Social Plugin