Na. Immaculate Makilika – MAELEZO
Rais Dkt. John Pombe Magufuli amewapa pole wananchi walioathiriwa na mafuriko yaliyotokea hivi karibuni mkoani Lindi.
Akizungumza jana (Jumatano, Januari 5, 2020) alipokuwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Kipindimbili, wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema kuwa Rais Magufuli anawapa pole wananchi waliokumbwa na mafuriko, huku akiwataka wananchi hao kuhama katika maeneo ya mabondeni.
“Pokeeni salamu za pole ninazozileta kwenu kutoka kwa Rais wetu mpendwa, Dkt. John Magufuli alizozitoa kwa wananchi wote mliokumbwa na mafuriko haya kwa kupoteza ndugu zenu wapendwa pamoja na mali”. Alisema Waziri Mkuu.
Aidha, Waziri Mkuu aliwataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kuhakikisha wananchi waliohamishwa kutoka mabondeni kwenda kwenye maeneo salama hawarejei tena, ili kunusurika na maafa ya mafuriko yanayoweza kujirudia kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini.
Waziri Mkuu alitembelea vijiji vingine vilivyokumbwa na maafa hayo ambavyo ni Nambilanje (Ruangwa), Nakiu na Njinjo (Kilwa) na Kitomanga (Lindi) ili kujionea athari za mafuriko na kuwapa pole wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, alisema mvua hizo zilizonyesha mfululizo zilisababisha maafa makubwa ambapo watu 21 walifariki huku wengine 26,481 katika kaya 4,344 wakikosa makazi.
Vilevile, Mkuu huyo wa Mkoa, alitaja maeneo yaliyoathiriwa na mvua hizo kuwa ni shule, zahanati, miundombinu ya barabara na mashamba.
Mkuu huyo wa Mkoa, alisema kuwa Ofisi yake ilipokea misaada ya vyakula, nguo, dawa na vifaa vya shule kutoka kwa wadau mbalimbali, pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Mafaa ambayo imetoa mahema 80, mablanketi 50, ndoo 1,500, mikeka 350 pamoja na vikombe 350.
Social Plugin