Rais Dkt. John Pombe Magufuli amewataka viongozi walioapishwa kufanya kazi kwa kufuata sheria na kanuni za uongozi pamoja na kuwa na hofu ya Mungu bila kusahau kutanguliza Uzalendo katika kuhakikisha Tanzania inafikia malengo iliyojiwekea.
Rais Magufuli Ameyasema hayo leo tarehe 3 Februari 2020 katika hafla ya Uapisho wa Viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni.
“Niwapongeze sana kwa majukumu yenu mapya ambayo nina amini mtakwenda kuyafanyia kazi kwa Uzalendo wa Kweli na bila Kusahau Kumtanguliza Mungu na kufanya kazi kwa kufuata sheria katika utendaji kazi wenu huko mnapoenda” amesema Rais Magufuli.
Sambamba na hilo Rais Magufuli ametumia fursa hiyo kumpongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi kwa utendaji kazi wake
katika kuisemea Serikali.
“Dkt. Abbasi umefanya kazi nzuri sana kwa kuisemea vizuri Serikali, nakupongeza sana kwa kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu hivyo utaendelea kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali hii mpaka atakapopatikana mtu mwingine “ amesema Rais Magufuli.
Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma amemshukuru Rais Magufuli kwa kujaza safu na kuteua Viongozi katika mahakama hivyo kwenda kurahisisha upatikanaji wa huduma.
“Nashukuru Rais magufuli kwa kuendelea kujaza safu za mahakama, umetupatia viongozi ambao wana weledi wa kazi hii ya mahakama, hivyo nina amini kabisa tunaenda kufanya kazi a kuwatumikia watanzania” amesema Jaji Mkuu.
Miongoni mwa walioapishwa leo na Rais Magufuli ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Hassan Abbasi, Katibu Mkuu wizara ya Nishati, Bi Zena Ahmed Said, katibu Mkuu Wizara ya Viwanda Riziki Shemdoe, Katibu Mkuu wizara ya mambo ya ndani ya Nchi Christopher Kadilo, Katibu Mkuu wizara ya Ardhi Bi
Marry Gaspar Makondo.
Wengine walioapishwa leo na Rais Magufuli ni Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Steven Mhoja Mashauri, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Emmanuel Mpawe Kukube, Naibu katibu Mkuu wizara ya nishati Leonard Robert Masanya.
Kwa upande kwa Mahakama Viongozi walioapishwa ni Msajili Mkuu wa mahakama ya Tanzania Wilbert Chuma, Msajili wa Mahakama ya Rufani Kelvin David, pamoja na Kamishna wa Magereza Brigedia Jenerali Suleiman Mzee na Kamishna wa Jeshi la zima moto na uokoaji John
Wiliam.
Social Plugin