RC SHINYANGA AMSIMAMISHA KAZI MTENDAJI WA KIJIJI CHA NYANDEKWA KAHAMA

 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack akizungumza na Watendaji wa kata, Maafisa Elimu kata na Wakuu wa shule za msingi na sekondari wa Halmashauri ya Mji Kahama leo tarehe 05/02/2020 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Anamringi Macha, kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kahama Bw. Anderson Msumba.
Maafisa Elimu kata, Watendaji wa kata, Wakuu wa shule wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa Mhe. Zainab Telack wakati wa kikao cha pamoja leo tarehe 05/02/2020 katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Mji Kahama.
***
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack ameiagiza Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Shinyanga kufanyia uchunguzi tuhuma zinazomkabili Afisa Mtendaji wa kijiji cha Nyandekwa, Halmashauri ya Mji Kahama Bw. Muhoja Malingumu za kupokea rushwa ili watoto wasiende shuleni.
Telack ametoa agizo hilo leo tarehe 05/02/2020 katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Mji Kahama ambapo amekutana na Watendaji wa kata, Maafisa Elimu kata na Wakuu wa shule za msingi na sekondari wa Halmashauri hiyo, akikamilisha ziara yake ya kukagua shughuli za Elimu Wilaya ya Kahama.
"Baadhi ya Watendaji wanashiriki kula rushwa ili watoto wasiende shule, sasa naanza na Mtendaji wa kijiji cha Nyandekwa, kuanzia leo namsimamisha kazi kwa kutuhumiwa kushiriki watoto wasiende shule, TAKUKURU mfanye uchunguzi. Mtendaji wa kata upo lakini huchukui hatua, humsaidii Mkuu wa shule, wewe pia ukibainika nakusimamisha kazi" amesema Telack akimtaka Mtendaji wa kata hiyo pia Bw. Makoye Kintuki kusimamia maendeleo ya shule.
Telacka amesema haivumiliki kuona baadhi ya watendaji wanajihusisha na vitendo vya rushwa ili watoto wasiende shule.
"Sisi tupo hapa ili watoto wasome, Mhe. Rais anatoa fedha nyingi kila mwezi, hatuwezi kuvumilia kuona vitendo hivi vinafanyika" amesema.
Katika kikao hicho pia, Telack amewahimiza Walimu kufanya kazi za halali za kuwaingizia kipato wakati wa muda wao wa ziada badala ya kutegemea mikopo ya riba kubwa na kuwaletea msongo wa mawazo, hatimaye wanashindwa kufundisha.
Amesisitiza Watendaji wote wanaosimamia Elimu warudi wakasimamie katika maeneo yao ili kuhakikisha ufaulu unapanda.
Bw. Mohamed Kahundi, Afisa Elimu Mkoa amewataka Maafisa Elimu kata kuhakikisha wanazingatia miongozo ya ratiba za vipindi kwenye shule zao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post